SIMBA NDIO TIMU KINARA KWENYE UTUPIAJI WA MABAO MPAKA SASA
Simba Sports Club imeendelea kuwa moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu ya NBC, ikijivunia rekodi ya mabao mengi baada ya kucheza mechi 13. Timu hiyo imefunga jumla ya mabao 29, huku mshambuliaji wao mahiri, Jean Ahoua, akiongoza orodha ya wafungaji kwa mabao sita.
Kwa upande mwingine, washambuliaji Ateba na Steven Mukwala wamechangia mabao manne kila mmoja, wakithibitisha ubora wa safu ya ushambuliaji wa Simba. Mechi ya kihistoria ya mzunguko wa kwanza ilifanyika tarehe 21 Desemba, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Kagera Sugar.
Simba pia inajivunia safu ya ulinzi imara, ikiwa imefungwa mabao matano pekee kwenye michezo yote, huku mlinda mlango Camara akifanikiwa kutoruhusu bao katika mechi 10.
Kwa sasa, Simba inaongoza msimamo wa ligi kwa alama 34, baada ya mechi 13. Wanapumulia nafasi ya pili ni Azam FC, wakiwa na alama 33 baada ya kucheza mechi 15.
Ikiwa na safu ya ushambuliaji na ulinzi thabiti, Simba inaonekana kuwa tishio kubwa msimu huu wa 2024/25 katika NBC Premier League.