KUHUSU YANGA KUFANYA VIBAYA SIKU HIZI….ALLY KAMWE AITAJA MAN CITY YA UK
LICHA ya kipigo cha mabao 2-0 ilichokipata juzi kwenye Uwanja wa Julai 5, jijini Algiers nchini Algeria dhidi ya MC Alger katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Klabu ya Yanga imesema haijakata tamaa kwani kuna pointi 12 zilizobaki za kupigania ambazo zinaweza kuifanya timu hiyo kusonga mbele kwenye Kundi A na kutinga hatua ya robo fainali.
Akizungumza nchini Algeria, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amekiri kuwa hali ni mbaya na wapo kwenye wakati mgumu, lakini amesema ndiyo mchezo wa soka ulivyo kwani hata klabu kubwa kama Machester City ya England, inapitia kipindi kama hicho.
“Hayakuwa matokeo rafiki na hatukujiandaa nayo, huwezi kwenda kwenye michuano mikubwa kama hii ukiwa na mategemeo ya kupoteza, lengo letu lilikuwa kushinda, lakini ndiyo maisha ya mchezo wa mpira wa miguu, ziko nyakati nzuri na zipo nyakati ngumu, sisi kama Yanga tunakiri sasa tupo katika nyakati ngumu.
“Tumeona hata Manchester City nayo haifanyi vizuri, inapitia kwenye wakati mgumu, kikubwa ni kurudi tena imara, haitakiwi hali hii kuendelea,” alisema Kamwe.
Alisema kilichobaki ni kujipanga ili kuzipata pointi 12 zilizobaki katika michezo minne iliyosalia nayo ili kuweza kupata nafasi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Naamini kwa ukongwe wa taasisi hii na uimara, tutarudi kwenye ubora wetu, matokeo haya yamemuumiza kila mtu, yamemuumiza mwalimu, benchi la ufundi, wachezaji na viongozi, lakini kwa kauli moja lazima tukubali ukweli, matokeo haya yanaweza kuikumba timu yoyote. Nyakati hizi zinapima watu uimara, wanachama na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuwa watulivu, tujiandae kwa mchezo unaofuata ili kurudi kwenye reli.
“Tunahitaji pointi 12 zilizobaki kusonga mbele, tunaamini tunaweza kuzipata kama tutajipanga,” alisema Kamwe.
Yalikuwa ni mabao ya Ayoub Abdellaoiu dakika ya 64 na Sofiane Bayazid dakika za nyongeza kabla ya mechi kumalizika, yaliifanya timu hiyo kupoteza mechi mbili mfululizo kwenye Kundi A, baada ya kupoteza kwa idadi kama hiyo ya mabao, Novemba 26, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kuendelea kuburuza mkia kwenye kundi.
Yanga sasa imebakisha michezo mitatu dhidi ya TP Mazembe utakaochezwa, Desemba 14, mwaka huu, nchini DR Congo na kurudiana Januari 3, ambapo Januari 10, itakuwa ugenini dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, kabla ya kumalizika mchezo wao wa mwisho nyumbani dhidi ya MC Alger, Januari 17, mwakani.