Klabu ya Manchester United imemteua Ruben Amorim kuwa kocha wao mpya akichukua nafasi ya Erik ten Hag ambaye amefurushwa klabuni hapo hivi karibuni.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye atatua Old Trafford kutoka klabu ya Sporting ya Lisbon mnamo Novemba 11, ametia saini mkataba hadi Juni 2027.
Mshambulizi wa zamani wa United, Ruud van Nistelrooy, ambaye alichukua jukumu la kuinoa klabu hiyo kwa muda baada ya Erik ten Hag kutimuliwa Jumatatu, atasalia kwenye mechi tatu zijazo za klabu hiyo.
Amorim, ni meneja wa sita wa kudumu United kuteuliwa tangu utawala wa miaka 26 wa Sir Alex Ferguson kumalizika na kustaafu mwaka 2013.
Katika taarifa, klabu hiyo ilisema kuwa “Ruben ni mmoja wa makocha wachanga wanaosisimua na wenye viwango vya juu katika soka la Ulaya”.
Mapema wiki, Sporting walisema kwamba United walikuwa wamekubali kulipa euro 10m (£8.3m) ili kuanzisha kipengele cha kutolewa katika kandarasi ya Amorim.
Mechi ya kwanza ya Amorim huko Manchester United inatarajiwa kuwa Novemba 24 dhidi ya Ipswich iliyopanda daraja, ambayo inakuja baada ya mapumziko ya kimataifa.
Mechi yake ya kwanza nyumbani itakuwa dhidi ya Bodo/Glimt ya Norway kwenye Ligi ya Europa mnamo Novemba 28, na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Everton wikendi inayofuata.