Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani kesho usiku kwenye Uwanja wa Chamazi Complex kucheza dhidi ya Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameanza kupanga mikakati ya kuongeza nguvu kikosini kwa kutaka kusajili wachezaji watatu wapya.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa Gamondi amewasilisha maombi kwa uongozi akipendekeza usajili wa nyota watatu mara dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa ili kuimarisha kikosi chake.
Chanzo chetu kimefichua kuwa Gamondi ameona upungufu katika nafasi za beki wa kulia, winga, na mshambuliaji wa kati.
“Kocha Gamondi ameona umuhimu wa kuongeza nguvu kikosini, na ametoa mapendekezo kwa uongozi kusajili wachezaji watatu wakati wa dirisha dogo, hasa kwenye nafasi alizoainisha, ili kuongeza mafanikio katika mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika,” kilieleza chanzo hicho.
Aidha, chanzo hicho kilisema kuwa kocha anatambua ushindani mkali wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa, hivyo anaona haja ya kuimarisha zaidi kikosi chake.
“Uongozi umeanza kufanyia kazi mapendekezo hayo, na mambo yanashughulikiwa kwa siri. Wachezaji wanaolengwa watakuwa wazi dirisha dogo litakapofunguliwa,” kiliongeza chanzo hicho.
Gamondi anataka kuboresha eneo la ushambuliaji, ambapo kwa sasa straika Clement Mzize na Mzambia Kennedy Musonda wamekuwa wakipata nafasi. Katika beki ya kulia, Yao Kwasi amekuwa chaguo la kwanza, ingawa mara nyingine Shomari Kibwana amekuwa akipewa nafasi.
Hivi karibuni, straika Kelvin Nashon alihusishwa na mazungumzo ya kujiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars, lakini mchezaji huyo amesema bado hajafanya mazungumzo yoyote na mabingwa hao watetezi.
Yanga pia inatazamia kujiimarisha kwa ajili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo imepangwa Kundi A pamoja na Al Hilal ya Sudan, TP Mazembe ya DR Congo, na MC Alger ya Algeria, kwenye mashindano yanayoandaliwa na CAF.