Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi, amesema kuwa iwapo kila mchezaji atajituma kwa kiwango cha asilimia 80, anaamini timu hiyo inaweza kushinda ubingwa msimu huu.
Akizungumza na gazeti la SpotiLEO, kocha huyo kutoka Morocco alieleza kuwa licha ya changamoto zilizopo kwenye ligi, amegundua baadhi ya wachezaji wake wamepoteza ari ya kupambana, hali iliyosababisha kukosa ushindi kwenye baadhi ya michezo.
“Hatuwezi kuangalia mechi za Simba na Yanga, tunahitaji kuinua ari yetu kama wanavyofanya wao. Baada ya kuona hili, nimezungumza na wachezaji wangu nikiwaomba kila mmoja kujituma kwa asilimia 80 ili kufanikisha kushinda ubingwa mwishoni mwa msimu huu,” alisema Taoussi.
Kocha Taoussi pia alieleza kuwa siri ya mafanikio ya Simba na Yanga ni wachezaji wao kujituma kwa ari ya juu kwenye kila mechi. Anataka wachezaji wake kuiga mfano huo msimu huu ili kufanikisha malengo yao. Ingawa Azam FC haijaanza vizuri msimu huu ikilinganishwa na wapinzani wake, Taoussi anaamini bado wanayo nafasi ya kurekebisha makosa na kuibuka mabingwa.
Kwa sasa, Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye ligi, ikiwa na pointi 15 baada ya mechi nane. Timu hiyo itashuka tena dimbani Oktoba 29, ikipambana na Ken Gold kwenye Uwanja wa Azam Complex.