WINGA wa Simba, Joshua Mutale hana noma na mtu, kila mchezaji ndani ya kikosi hicho ni mshikaji wake, hapendi kununa, badala yake kila anapokuwepo lazima aache kicheko kwa wengine.
Alipoulizwa Mutale mara nyingi kwa nini anaonekana akiwachekesha wachezaji wenzake je, ana mpango huko baadaye kuwa mchekeshaji? Naye amejibu; “Sina mpango kabisa, ila ninapokuwa na wenzangu napenda kuwaona wana furaha, kwani sio muumini wa kuwa sababu ya wengine kununa.”
“Katika maisha yangu, nimechagua kuyapa nafasi mambo ambayo yanaufurahisha moyo wangu, ndio maana muda mwingine nikiwa napumzika, nawaangalia wachekeshaji kutoka Nigeria, ndio maana mnaona muda wote natabasamu,” ameongeza nyota huyo kutoka Zambia.
Mutale alifichua ndani ya kikosi hicho, kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma ni mchekeshaji wa chini chini, tofauti na watu wanavyomuona ana sura ya ukimya.
“Kagoma wakati mwingine akinifundisha Kiswahili ananiambia maneno mabaya, nikimuuliza Steven Mukwala nimeambiwa hivi, hilo neno lina maana gani, ananiambia sio neno zuri usilitumie na ananiambia maana yake, nikirudi kwa Kagoma kwa nini unanifundisha vitu vibaya anaishia kucheka tu,” alisema Mutale ambaye Simba ilimsajili kutoka Power Dynamos ya Zambia.
Mbali na uchekeshaji alionao, Mutale amekiri Ligi Kuu ni ngumu, inayohitaji kujituma kwa bidii kuyafikia malengo ya kuchukua ubingwa.
“Kwa mechi ambazo tumecheza za Ligi Kuu, zimenipa picha jinsi ambavyo ni ngumu na ina upinzani wa juu, ndio maana nasisitiza tunahitaji kujituma kwa bidii,” amesema.