AZAM FC HAITAKI UTANI, KAZI DAKIKA 270
UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa kwenye mechi zijazo watapambana kufanya vizuri kupata pointi tatu muhimu ndani ya uwanja msimu wa 2024/25 ambao una ushindani mkubwa.
Funga kazi ndani ya Azam FC kwa Septemba 29 ilikuwa dhidi ya Mashujaa ugenini baada ya dakika 90 ubao wa Lake Tanganyika ulisoma Mashujaa 0-0 Azam FC hivyo waligawana pointi mojamoja kwenye mchezo huo.
Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC amesema kuwa wanaamini watakuwa na mwendelezo mzuri kwenye mechi zijazo hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nao kila hatua.
“Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi tunahitaji ushindi kwenye mechi zetu ambazo tunacheza hilo linawezekana kutokana na utayari wa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuwa imara kwenye kuwapa mbinu wachezaji wetu wote.”
Mechi tatu zitakuwa zinawahusu ndani ya Oktoba ambazo ni dakika 270 kwenye msako wa pointi tisa ambazo wapinzani wao nao wanazipigia hesabu pia.
Ikumbukwe kwamba Mzizima Dabi ya Azam FC v Simba mzunguko wa kwanza ulikamilika kwa ubao wa Uwanja wa New Amaan Complex kusoma Azam FC 0-2 Simba.
Oktoba 3 2024 : Namungo v Azam FC itachezwa saa 3:00 usiku, Uwanja wa Majaliwa. Oktoba 18 2024: Prisons v Azam FC, Uwanja wa Sokoine, saa 10:00 jioni. Azam FC v Ken Gold, saa 1:00 usiku itakuwa Oktoba 29 2024, Azam Complex.
Matajiri Azam FC mechi mbili ambazo ni dakika 180 watakuwa ugenini na mchezo mmoja watakuwa kwenye ngome yao kongwe pale Uwanja wa Azam Complex.