BEKI wa JKT Tanzania ambaye alipata nafasi ya kucheza Yanga, David Bryson amemtaja Kibwana Shomari kuwa ni beki mzuri lakini anapotezwa na uwepo wa Attohoula Yao.
David Bryson amesema kuna mabeki wengi namba mbili wanaocheza ligi ya ndani anaowakubali akiwemo Kibwana, lakini anajisikia vibaya kuona licha ya kucheza kwa mafanikio Yanga anakosa nafasi ya kucheza mbele ya Yao.
“Ni kweli kuna utofauti wa uchezaji, lakini Kibwana akipewa nafasi ni aina ya mabeki wanaofanya vizuri anaweza kutengeneza mashambulizi lakini pia ana kasi ya kushuka kusaidia kukaba kama ilivyo kwa Yao,” amesema.
“Kinachomtokea ni sawa na mimi nilivyokuwa Yanga ujio wa Joyce Lomalisa ulinifanya niombe kuondoka ili nikatafute changamoto nyingine sasa nafurahia maisha ndani ya JKT Tanzania nacheza.”
Bryson amesema wachezaji wa kigeni wanakuja kuwaongeza changamoto, lakini haina maana kwamba hawana nafasi ya kuonyesha na kufanya vizuri, hivyo anaamini endapo Miguel Gamondi akimpa muda Kibwana kucheza hata kwa dakika chache ili kuendelea kumjenga na kumuweka katika nafasi.
“Sina maana kwamba kuna utofauti wa ubora, lakini naamini wachezaji wa kigeni wanapewa kipaumbele cha kucheza kutokana na kusajiliwa kwa fedha nyingi tofauti na sisi japo kuna wengine uwezo wao ni mkubwa na wamekuwa wakitupa somo la kupambana,” amesema na kuongeza:
“Nakumbuka kipindi nipo Yanga nilimkuta Lomalisa (Joyce) alikuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara nilipambana kuonyesha (uwezo), lakini haikuwa rahisi kwangu kucheza ndipo nilipoamua kutafuta mlango wa kutokea kwa kuomba niondoke ili nikatafute changamoto nyingine nje ya Yanga. Sasa nacheza JKT Tanzania na nafurahia maisha ya hapa.”
Ujio wa Yao ndani ya Yanga, Kibwana ambaye amecheza kwa mafanikio misimu miwili mfululizo akiisaidia kutwaa mataji umekuwa mwiba kwake kwani hachezi na amekuwa akikalia benchi ambapo mara ya mwisho alionekana kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya TS Galax nchini Afrika Kusini.