Kikosi cha Taifa Stars kiliondoka nchini jana kwenda Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wa pili wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 utakaopigwa keshokutwa dhidi ya Guinea, huku kocha akiamini watafanya vizuri.
Akizungumzia maandalizi kabla ya timu kupaa, kaimu kocha mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema baada ya mchezo dhidi ya Ethiopia walifanya tathimini ya kikosi na kurekebisha upungufu uliojitokeza na sasa wanaenda kupambana kusaka pointi ugenini..
“Kila mmoja wetu yupo tayari kwa changamoto nyingine. Ni mchezo mgumu sana kwa sababu tunakutana na wapinzani ambao wamepoteza mechi ya kwanza, hivyo haitakuwa rahisi. Shida kubwa kwetu ilikuwa ni umaliziaji na tumefanyia kazi hilo,” alisema.