KITAIFA

SIMBA YAPIGA HESABU KULIPA KISASI KWA MKAPA

UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa mpango mkubwa kwenye anga la kimataifa ni kulipa kisasi kwa wapinzani wao Al Ahli Tripoli kwa mashabiki kujitokea kwa wingi kwenye mchezo wa marudio ili kuwaongezea nguvu wachezaji wa timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Septemba 22 2024 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa wakiwa na kumbukumbu ya kutoshana nguvu kwenye mchezo uliopita wakiwa ugenini kwa ubao kusoma 0-0.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amebainisha kuwa mchezo wa Jumapili ni muhimu kupata matokeo na mashabiki wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuwashangilia wachezaji mwanzo mwisho kulipa kisasi cha ugenini ambapo mgeni rasmi kwenye mchezo huo atakuwa kiungo Yusuph Kagoma.

“Kwa sasa tupo nyuma mabao 2-0 dhidi ya mashabiki wa Al Ahli Tripoli. Bao  la kwanza kuujaza uwanja wao wote kwa mashabiki 50,065. Hili kwetu ni deni na sisi kuujaza. Sina hofu na hilo kujaza Uwanja wa Mkapa. Wao walijaa na sisi tunapaswa kujaa. Bao la pili mashabiki wote kuvaa jezi za timu yao, na hilo tuna wajibu wa kwenda kusawazisha. Kila Mwanasimba atakayekuja uwanjani anatakiwa kuvaa jezi mpya ya msimu hii.

“Kwa kutambua kwamba tunapaswa kuvaa jezi za aina moja, mdhamini wetu wa jezi amepunguza bei kwa punguzo maalumu. Jezi zitauzwa Tsh. 30,000 na zinapatikana kwenye maduka ya Sandaland The Only One lakini pia kwa atakayekuja uwanjani na kununua jezi yake ya Tsh. 30,000 atampa zawadi ya tiketi ya mchezo bure.

“Tunapohimiza watu wavae jezi, tunahimiza watu wavae jezi orijino. Tuseme wazi kwamba tayari tuna taarifa ya mzigo wa jezi feki kuingia nchini. Mdhibiti wa kwanza wa jezi feki ni wewe Mwanasimba, usikubali kununua jezi ya aina hiyo.

“Ili kupendezesha uwanja. Wanaume wote siku ya Jumapili tutavaa jezi nyekundu, wanawake wote watavaa jezi nyeupe na watoto wote wa Simba watavaa blue. Kama huna jezi nyekundu na wewe ni mwanaume kanunue jezi mpya na kama wewe ni mwanamke huna jezi nyeupe kanunue jezi mpya kwa bei ya punguzo.”

Kaulimbiu kuelekea mchezo huo wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi inasema “Tutawakaanga”.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button