Kama uliona bado mapema kwa Simba kutafuta mchezaji wa kumsajili dirisha dogo msimu huu, basi umekosea, kwani Wekundu hao wamegonga hodi tena kwa Winga Mkongoman Elie Mpanzu.
Winga huyo aliyekuwa akiichezea AS Vita kabla ya kutimkia Ubelgiji, aliwahi kuhitajika na Simba lakini aliamua kuwakacha kweupe akitoa sababu za kufanya hivyo ikiwamo ishu ya kutaka kucheza soka Ulaya, lakini mabosi wa Msimbazi wameamua kumrudia tena.
Inaelezwa Simba imerejea tena kwa winga huyo, baada ya kuona kikosi hicho kinahitaji nguvu hasa eneo la kushoto, na mchezaji huyo kuonekana kama amechemka huko Ubelgiji.
Taarifa za ndani kutoka klabu ya Simba zikieleza kuwa, hatua ya kumrudia Mpanzu imetokana baada ya kugundua kuwa kuna mahali panavuja hasa eneo la winga. “Kuna mchezaji mmoja itabidi atolewe kama dili la Mpanzu litatiki ili kutimiza kanuni ya kuwa na wachezaji 12 wa kigeni. Hatuwezi tukasema atakuwa nani kwani bado ni mapema lakini kocha ndiye mwenye maamuzi juu ya hili, hivyo ataongea na uongozi juu ya nani apunguzwe,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.