UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji wataukabili kwa hesabu kubwa ya kupata pointi tatu kutokana na muda kuwa mchache kwenye maandalizi.
Ni ushindi dhidi ya Azam FC ilipata kwenye mchezo wa Mzizima Dabi uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Septemba 26 mchezo ulichezwa na Septemba 27 kikosi kilirejea Dar, leo Septemba 28 2024 kikosi kimetua Dodoma kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji kwa kuwa wanatambua umuhimu wa pointi tatu kwenye mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa.
“Tumemaliza mchezo wetu dhidi ya Azam FC na kupata ushindi hapo hesabu ni kushinda mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji, hakika huu ni mchezo muhimu hilo tunatambua lakini hesabu nzito zipo kwenye kupata pointi tatu muhimu.
“Unaona kwenye mechi za ligi tumepata ushindi katika mechi zetu tatu mfululizo huu ni mwanzo mzuri na sasa tunahitaji mwendelezo huo uendelee, mashabiki wa Simba wa Dodoma wamekuwa wakitushangilia mwanzo mwisho na hata pale ambapo hatukuwa imara msimu uliopita bado walikuwa pamoja nasi.
“Kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Dodoma Jiji tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani kutushangilia bila kuchoka hakika watafurahi vibaya mno.”
Simba imekusanya pointi 9 baada ya kucheza mechi tatu na safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 9 ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila baada ya mchezo mmoja.