TANZANIA leo itashuka kwenye Uwanja wa Charles Konan Bannyo, uliopo mjini Yamoussoukro nchini Ivory Coast kucheza mchezo wa pili wa Kundi H, katika kampeni yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco, dhidi ya Guinea.
Mechi hiyo itakayopigwa saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania, inachezwa nchini humo kutokana na nchi ya Guinea kutokuwa na viwanja vinavyokidhi viwango vilivyowekwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa ajili ya mechi za kimataifa inazozisimamia.
Mchezo huo unachezwa siku sita tu baada ya Stars kulazimishwa suluhu nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Timu ya Taifa, Ethiopia.
Stars inacheza na timu ambayo katika mchezo wa kwanza ilipata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemomkrasia ya Congo, ikiwa ugenini.
Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na hakina majeruhi yeyote, huku akisisitiza kuwa mchezo wa leo wataingia na mbinu tofauti na walivyocheza Dar es Salaam, kwani watashambulia zaidi ili kupata pointi tatu ambazo zitawafanya kukaa sawa kwenye msimamo wa kundi hilo.
“Vijana wetu wapo tayari, tunajua mechi hii ni ngumu, haya ni mashindano ya kufuzu AFCON, kila timu inajitahidi ili ifuzu na nchi zao pia wamezipa umuhimu mkubwa, lakini tutapambana.
“Wenzetu hawa walianza vibaya mechi ya kwanza, walifungwa bao 1-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, sisi hatukufanya vibaya sana tumetoka suluhu, kwa hiyo malengo yetu ni kushinda mechi hii,” alisema Morocco.
Kocha huyo ametaja mfumo na mbinu atakayotumia kwenye mchezo wa leo kuwa ni wa kushambulia zaidi
“Tutashambulia zaidi, huo ndiyo mfumo tutakaotumia, kwa sababu hakuna kingine tena, tunahitaji pointi tatu. Mpira siku hizi unachezwa popote pale, kwa jinsi tulivyocheza mechi iliyopita kipindi cha pili na tumerekebisha na makosa tuliyoyaona, tuna uhakika wa kushinda,”alisema Morocco.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, alisema wachezaji wako vizuri na wamezungumza nao, ambapo wamewaahidi kulipambania taifa kwa kucheza kwa juhudi zao zote kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
“Wachezaji wetu wapo sawa, lakini kwenye soka matokeo yoyote yanaweza kutokea, hata hivyo tuna wachezaji ambao ni wazoefu kwenye michuano hii, kisaikolojia wapo sawa, hakuna aliyepata mshtuko eti kwa sababu tumepata sare nyumbani katika mchezo uliopita, tumekuwa tukizungumza nao na wametuhakikishia kufanya vizuri,” alisema.