KINA MAGOMA NA YANGA KWENDA MAHAKAMANI TENA LEO, KUONA UAMUZI UTAKAVYOKUA
Hatima ya uhalali wa rufaa dhidi ya Klabu ya Dar es Salaam, Young African Sports, maarufu Yanga, inatarajiwa kujulikana leo Jumatatu, Septemba 9, 2024, wakati Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, itakapotoa uamuzi wa pingamizi dhidi ya rufaa hiyo.
Rufaa hiyo imefunguliwa na Juma Ally Magoma na mwenzake Geoffrey Mwaipopo, wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kuiongezea Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo na wenzake muda wa kufungua shauri la maombi ya marejeo.
Klabu hiyo iliomba kuongezewa muda huo ili kufungua shauri hilo la marejeo au hukumu ya mahakama hiyo iliyobatilisha Katiba yake ya sasa kufuatia kesi ya msingi iliyofunguliwa na Magoma na mwenzake, wakihoji uhalali wa katiba hiyo.
Magoma na Mwaipopo ambao wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo, hawakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu kuiongezea muda bodi hiyo ya Yanga kufungua shauri hilo la marejeo, hivyo wakakimbilia Mahakama Kuu ambako walikata rufaa hiyo.
Wajibu rufaa katika rufaa hiyo ni Bodi hiyo ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga (mjibu rufaa wa kwanza), Fatma Abeid Karume (mjumbe wa bodi hiyo mpaka sasa), Abeid Abeid na Jabiri Katundu, ambao pia waliwahi kuwa wajumbe wa bodi ya klabu hiyo.
Bodi ya wadhamini wa Yanga imewawekea pingamizi la hoja za kisheria kina Magoma dhidi ya rufaa hiyo, ikibainisha hoja mbili. Kwanza inadai uamuzi ambao kina Magoma wameukatia rufaa na ya pili wanadai rufaa hiyo imeshapitwa na tukio.