Wakati mashabiki wa Yanga wakitambia kikosi chao kushinda kwa idadi kubwa ya mabao dhidi ya Ken Gold, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema anachotaka ni pointi tatu, lakini wapinzani wao wakijichanganya watawapiga nyingi.
Yanga imekuwa na matokeo mazuri huku ikiwa na mwendelezo bora katika ufungaji mabao baada ya kutupia 19 katika mechi tano ilizocheza nyuma ikiwamo ya klabu bingwa Afrika.
Katika mchezo wa mwisho imefunga mabao sita wakati ikiiondoa CBE katika hatua za awali ligi ya mabingwa Afrika na kesho Jumatano itawavaa Ken Gold wanaochechemea mkiani bila pointi baada ya kupoteza michezo minne mfululizo.
Akizungumzia mchezo huo hii leo, Gamondi amesema kiu yake katika mchezo huo ni kupata pointi tatu bila kujali idadi ya mabao akieleza kuwa iwapo itatokea kupata nafasi ya kutupia zaidi ya manne itakuwa bora zaidi na hawataacha kufanya hivyo.
Amesema wanaoibeza Ken Gold kwa matokeo waliyonayo, kwake ni tofauti kwakuwa anaamini ni timu nzuri iliyopanda Ligi Kuu hivyo mbinu alizotumia katika michezo iliyopita haitabadilika sana kutokana na wapinzani watakavyokuwa.
“Mimi kiu yangu ni Yanga kupata pointi tatu hata kwa bao moja ni sawa, ila kama tutapata nafasi ya kufunga zaidi tutafanya hivyo na itakuwa nzuri zaidi, nimewaandaa vyema wachezaji wangu” amesema Gamondi.
Kocha huyo ameongeza kuwa wachezaji wote walosafiri wako fiti isipokuwa wanamkosa Farid Mussa ambaye ni majeruhi, akieleza kuwa Yanga inao nyota wengi na wenye uwezo hivyo wanasubiri muda ufike waingie uwanjani.
Kuhusu ratiba yao na hali ya uchovu, Gamondi amesema hana hofu yoyote kwani wachezaji wake wanao uzoefu na uwezo binafsi na anachoweza kufanya ni kufanya maboresho kujua nani aanze au kusubiri.
“Ni juzi tumecheza mechi ya klabu bingwa na kesho tuko uwanjani, sina hofu yoyote na badala yake nitaangalia nani aanze au kusubiri kutokana na upana wa kikosi changu binafsi nafurahia ratiba,” amesema kocha huyo.
Kwa upande wake nyota wa timu hiyo, Aziz Andambwile amesema licha ya ubora walionao, lakini hawawezi kuwadharau Ken Gold badala yake watapambana kupata ushindi ili kujiweka pazuri.
Amesema wanafahamu kilichowahi kuwakuta mkoani Mbeya, Yanga alipopoteza mechi zake dhidi ya Ihefu kwa misimu miwili mfululizo, hivyo watakuwa makini na tahadhari kubwa kufikia malengo.
“Lazima tuwaheshimu wapinzani kwakuwa historia tunaikumbuka, tutacheza kwa umakini kulingana na kocha alivyotuelekeza kuhakikisha pointi tatu tunaondoka nazo na kujiweka pazuri,” amesema mchezaji huyo kiraka.