Klabu ya Azam FC inaelezwa kuwa kwa sasa nguvu imehamishiwa kwa Mkongoman, Florent Ibenge wa Al Hilal Club mwenye CV kubwa Afrika. Uongozi wa timu hiyo, unadaiwa kuanzisha mchakato wa haraka wa kuzungumza na Ibenge, ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akihusishwa na klabu mbalimbali za hapa nchini kama Simba na Yanga.
Chanzo cha ndani cha klabu hiyo, kinasema mazungumzo baina ya Azam na Ibenge yanaendelea na pesa siyo ishu kwao, lengo ni kujenga timu ya kunyakua mataji na kufanya vizuri kimataifa, viongozi wanaamini jukumu hilo kocha huyo analiweza. “Mazungumzo yanaendelea baina yetu na Ibenge, kwani awali tulianza na Nabi ambaye licha ya kumpa pesa ndefu aliikataa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“CV ya makocha ambao tumewafuata ni kubwa mfano Nabi aliijenga Yanga ndio maana hadi leo inafanya vizuri, ukija kwa Ibenge anachokifanya katika timu mbalimbali za Afrika ni kikubwa, endapo dili likikamilika tutafurahi na tutaona hatua ya malengo yetu.”
Kwa sasa Ibenge yupo nchini na timu ya Al Hilal ambayo juzi jioni ilitoka sare ya 1-1 na Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa uliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC.