EDO KUMWEMBE: HAMZA NI BEKI BORA SANA JAPO HAIMBWI
Tuna kijana wetu, Hamza Abdulrazak. Beki wa mpira. Mtulivu kama alivyo. Anacheza mpira wa miaka ya mbele yake. Simba imejipiga chenga ya mwili na Hamza ameokoa jahazi. Simba walimsajili beki, Chamou Karaboue kutoka Asec Mimosas wakiamini angetengeneza pacha nzuri na Che Malone. Hata hivyo Hamza ameingia kati.
.
Kwa macho yangu Chamou ni mzito. Ana umbo kubwa, lakini kwa mechi za kwanza ambazo nimemuangalia sijaona kama anaweza kufikia ule uwezo wa kina Josh Onyango na Serge Wawa katika ubora wao. Kabla mambo hayajaharibika mbeleni Hamza amejitokeza kuokoa jahazi.
.
Hakusajiliwa kwa mbwembwe sana lakini ghafla ameibuka kuwa tumaini. Hamza ana kimo kizuri. Ana utulivu, ana akili ya mpira, ana nguvu, ana kila kitu. Moyo wangu unapata liwazo ninapojikumbusha kwamba safu ya ulinzi itaendelea kuwa salama kwa muda mrefu ujao.
.
Tuna kina Dickson Job, Bakari Mwamunyeto, Ibrahim Bacca. Tuna Hamza pia. Kuna wakati aliwahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa. Hatujui kwanini hakuendelea kuitwa. Hata hivyo muda mchache ujao anaweza kuitwa.
— Legend, Edo Kumwembe.