WANARIADHA WA TANZANIA WATUA KUSHIRIKI OLIMPIKI
Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) Henry Tandau amewapokea wanariadha wanne wa Tanzania watakaoshiriki katika mbio za Marathon za mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 siku za Jumamosi na Jumapili.
Wanariadha hao waliowasili usiku huu katika Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle ni nahodha wa timu ya Taifa ya riadha Alphonce Felix Simbu, Gabriel Gerald Geay, Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri. Wakimbia hao wa Marathon kwa wanaume na wanawake mtawalia wametua na kocha wao Anthony Njiku Mwingereza aliyekuwa akiwanoa kambini Arusha.
Wakimbiaji wanaume Simbu na Geaye, ndio watakaoanza kukimbia siku ya Jumamosi asubuhi huku wakimbiaji wanawake, Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri wamepangwa kukimbia Agosti 11, 2024, ambayo ndiyo itakuwa siku ya mwisho ya Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.