Azim Dewji ametoa tahadhari kwa mashabiki wa Simba na Yanga kuacha kwenda na matokeo yao mfukoni, kwani mechi za Dabi huwa hazitabariki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Dewji, ambaye aliifadhili Simba miaka ya 1990, na kuiwezesha kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali, ikiwamo kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pia Kombe la Kagame na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, CAF, wakati huo likiitwa Kombe la CAF mwaka 1993, amesema kwa uzoefu wake katika masuala ya soka, hasa kwenye mechi za dabi kati ya Simba na Yanga matokeo yanaamuliwa na dakika 90 tu za mchezo, na wala si ubora wa kikosi kwa wakati husika.
Alisema ni kweli kuna wakati ubora huamua mechi hizo, lakini mara kwa mara imetokea Simba dhaifu kuifunga Yanga bora na Yanga ambayo haipo vizuri msimu huo kuifunga Simba iliyo kwenye kiwango cha juu.
“Dabi haina mwenyewe, matokeo yanategemea uwezo wa siku hiyo tu jinsi wachezaji watakavyopambana, timu gani wachezaji wale wameamka vizuri, au mbinu za walimu, huwezi kusema eti Simba watafungwa kesho kutwa, mechi za dabi hazitegemei hivyo, haiangaliwi timu gani bora,” alisema Dewji ambaye alitamba akiwa Simba huku upande wa Yanga kukiwa na marehemu, Abbas Gulamali, aliyekuwa mfadhili wa Yanga na Mbunge wa Jimbo la Kilombero.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana kesho, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mechi ya Ngao ya Jamii, kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu.
Akizungumzia timu hizo mbili, Dewji alisema zote zina wachezaji wazuri kwa jinsi walivyoziona kwenye Simba Day na kilele cha Wiki ya Mwananchi, lakini Simba inahitaji muda ili wachezaji wake wazoeane zaidi kabla ya kuwa tishio.
“Yanga na Simba zina wachezaji wazuri, lakini Simba wanatakiwa kukaa na kuelewana kwanza, timu yoyote ili iwe nzuri ni lazima kwanza ikae pamoja wachezaji wazoeane.
Simba ina wachezaji 13 wote ni wapya kwenye kikosi, hivyo itawachukua muda mpaka kukaa vizuri, alibainisha.
Mwanamichezo huyo pia alionyesha kutoridhishwa na timu zote mbili kutokuwa na wachezaji wengi wa Kitanzania, tofauti na timu ya Red Arrows ya Zambia na APR ya Rwanda ambazo zilikuwa na wazawa wengi kuliko wageni.
“Haswa wale Wazambia, walikuwa na asilimia 90 wachezaji wa Kizambia, sijui wachezaji wetu wanakosea wapi?” alishangaa.
Hata hivyo akakumbuka kuwa huko nyuma michezo iliondolewa shuleni, ni hivi karibuni tu ndiyo imerudishwa.
“Mimi naona tulifanya makosa kuondoa mpira shuleni, kule ndiyo unaanza kuona kipaji cha mchezaji, siku hizi naona wamerudisha, sasa tuangalie miaka kadhaa ijayo,” alisema Dewji.