AHOUA ASEMA “NIMEWASIKIA SASA SUBIRINI KAZI”
Kama ulimchukulia poa kiungo mpya wa Simba, Jean Charles Ahoua ulikosea kwani sasa ameanza kuuwasha moto ndani ya mechi mbili tu za Ligi Kuu, na tayari ameahidi kuwa rekodi ndizo zitazungumza.
Ahoua katika msimu wa 2023/24 aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Ivory Coast (MVP), akifunga mabao 12 na kutoa asisti tisa. Tangu alipotua nchini amecheza mechi mbili za ligi akiwa na asisti tatu na bao moja huku akishiriki katika mabao mawili kati ya manne iliyofunga Simba dhidi ya Fountain Gate, juzi katika ligi.
“Mabadiliko ndiyo yalinichelewesha kwa kuwa timu ni mpya, lakini kuanzia sasa nataka kuwafurahisha Wanasimba kwa sababu najua kwamba baadhi ya watu walikuwa hawanizungumzi vizuri kwa kuwa nilichelewa kuanza kufunga, lakini haikuwa inaniumiza kwani nilijua tu baada ya muda watanijua mimi ni nani,”
“Simba ina timu na makocha wazuri lakini tunahitaji muda na tunavyoendelea kuwa pamoja kuna kitu kikubwa tunakijenga na baada ya muda mfupi matokeo yataonekana,”
“Binafsi ninapenda kutangulia kwanza kuwatengenezea nafasi washambuliaji kwa kutoa asisti, lakini kama nitapata nafasi nitafunga kwa kuwa najua kufunga.” alisema Ahoua.