KINDA jipya la Azam FC raia wa Mali, Cheickna Diakite limeweka wazi kwamba huenda mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ulioikutanisha timu aliyokuwa akiichezea ya AS Real Bamako dhidi ya Yanga msimu wa 2022–2023, ndiyo iliyomfanya atue nchini kukipiga kwa matajiri hao wa Chamazi.
Winga huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu alisema, wakati timu ya AS Real Bamako inatua nchini ndipo baadhi ya viongozi mbalimbali walianza kumfuatilia katika mchezo wao na Yanga na ndipo Azam ilipoonyesha nia ya kumhitaji.
“Nakumbuka katika mchezo huo nilianzia benchi lakini wakati nilipoingia nilionyesha kiwango kizuri ambacho kiliwavutia baadhi ya mashabiki na viongozi mbalimbali, kwangu ilikuwa kama faraja kwa sababu tulipoteza tukiwa ugenini,” alisema.
Diakite aliongeza, asingependa kufananishwa na winga aliyeondoka ndani ya kikosi cha Azam, Kipre Junior aliyejiunga na MC Alger ya Algeria, kwani kila mmoja ana aina yake ya uchezaji, na ana heshimu uwezo na mchango mkubwa wa nyota huyo.
Katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Fiston Mayele na Jesus Moloko, mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 8, 2023.
Msimu huo Yanga iliongoza katika kundi ‘D’ katika michuano hiyo baada ya kukusanya jumla ya pointi 13 sambamba na US Monastir ya Tunisia ila zilitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa huku AS Real Bamako ikishika nafasi ya tatu kwa pointi tano.
TP Mazembe ya DR Congo iliburuza mkia kwa pointi tatu, huku Yanga ikifika hadi fainali ya michuano hiyo msimu huo ikilikosa taji kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini mbele ya USM Alger baada ya kupoteza Kwa Mkapa kwa mabao 2-1 kisha kushinda ugenini kwa bao 1-0 na matokeo kuwa 2-2.