MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amefafanua juu ya sintofahamu kuhusu usajili wa aliyekuwa kiungo wa KMC FC, Awesu Awesu.
Kuna taarifa iliibuka kutoka kwa viongozi wa KMC FC baada ya Simba kumtambulisha Awesu kuwa klabu hiyo haijafuata taratibu za usajili na kwenda mbali kuwa bado ni mchezaji wao.
Ahmad amesema viongozi wa Simba wako makini katika usajili wao na alifika mbali na kuhoji kwa nini sajili ya ndani ziwe na kelele na kuonekana wanafanya uhuni, wamefuata taratibu zote za usajili kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa 2024/25.
“Sajili za ndani ndio ziwe na kelele, kwa nini isiwe usajili wa nyota wa kigeni tumemsajili Debora Fernandes, Augustine Okejepha , Joshua Mutale na wengine lakinu hakuna hizo kele za kuwa Simba ni wahuni.
Simba hawafanyi uhuni, bali tunaofanya nao kazi ndio wanaleta uhuni, tuweza kufanya usajili wa mchezaji kutoka Ivory Coast au Ghana tushinde kujua utaratibu wa nyota mzawa,” amesema Ahmed.
Ameshusha presha ya mashabiki wa klabu hiyo kuwa wachezaji wote ambao wamewasajili wamefuata taratibu zote za usajili na suala la Awesu limekamilika kisheria na taratibu zote za usajili.
Kuhusu suala la Aubin Kramo, Ahmed amesema nyota huyo hayupo kwenye mipango ya Simba kwa msimu wa 2024/25 kwa sababu ya tathimini ya kimatibabu na kiufundi kuona hataweza kuwezana na presha ya mashabiki wa Simba kwa msimu mpya.
“Kramo ametoka katika majeraha makubwa na kutokana na msimu huu utakuwa wa presha kutwa tumeona bora kumtafutia timu aende kwa mkopo au kuachana naye. Maana hataweza presha za mashabiki wanachokihitaji ni ubingwa tu,” amesema Ahmed.