LICHA ya kupata dili la kuichezea G.D. Sagrada Esperanca ya Angola, beki wa kushoto aliyeachwa Yanga, Joyce Lomalisa amelia na mabosi wa klabu hiyo ya Jangwani kwa kumwekea kauzibe kupata ofa nzuri kwa timu zilizokuwa zikimpigia hesabu kumsajili kabla ya Waangola hao kumrudia katika Ligi ya Girabola.
Lomalisa alisema alikuwa anatamani sana kusalia Jangwani, lakini mambo yalitibuka na kinachomuuma ni kuchelewa kupatikana kwa muafaka wa kuachwa aondoke kuliko mkosesha dili nyingi.
Beki huyo aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili, amejiunga na Sagrada Esperanca, aliyokuwa akiitumikia kabla ya kujiunga na Yanga, pia akiwahi kuitumikia Inter Club pia ya huko huko Angola mbali na AS Vita kwa DR Congo anakotokea nyota huyo.
Akizungumzia mustakabali wake Lomalisa alisema, amerudi Angola kwa kuwa ni kama nyumbani kwake japo alitamani kubaki Tanzania.
“Yanga walinionyesha nia ya kunibakisha nikapotezea ofa, wakageuka.”
Yanga iliachana na beki huyo wa kushoto muda mchache kisha wakamtambulisha Mcongo mwenzake, Chadrack Boka kutoka FC Lupopo.
Akiwa na Yanga aliyodumu nayo kwa misimu miwili Lomalisa ameicheza klabu hiyo kwa mafanikio makubwa sana, huku yeye akiwa moja ya mabeki bora wa pembeni.
Katika misimu yake miwili alifanikiwa kuvaa medali nyingi, ikiwemo za Ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC mara 2, Kombe la Shirikisho la CRDB mara 2, Ngao ya Jamii 1, Mapinduzi mara 1 na medali ya washindi wa pili Kombe la Shirikisho Afrika.