KUMBE BADO AZIZ KI HAJASAINI MKATABA, ATOA MASHARTI MAZITO
Inadaiwa kuwa Klabu ya Yanga imefikia makubaliano ya kumuongeza mkataba wa kusalia klabuni hapo kiungo wao Stephane Aziz Ki ambaye ametoa masharti kwa uongozi wa klabu, kubwa akihitaji kurejeshwa kwa kiungo mwenzake wa kimataifa wa Burkinafaso, Yacouba Sogne.
Ikumbukwe kuwa Aziz Ki alitua nchini kuchukuwa nafasi ya Yacouba ambaye aliandamwa na majeraha na kumpisha mfungaji bora huyo wa msimu uliomalizika ambaye mkataba wake umefikia tamati na inalezwa kuwa tayari amekubali kusaini mkataba mwingine.
Taarifa zilizotufikia kuwa nyota huyo amewapa masharti ya kutaka kuongezewa dau la usajili pamoja na mshahara kubwa pamoja na kurejeshwa kwa Yacouba.
“Ni kweli bado Aziz Ki hajaongeza mkataba na Yanga, licha ya kuwepo kwa mazungumzo hayo ya kuendelea kusalia ndani ya timu hiyo, kuna mambo ametaka kufanyiwa ikiwemo kurejea kwa rafiki yake ndani ya kikosi hicho,” kimesema chanzo chetu cha habari.
Amesema tayari injinia Hersi ameridhia baadhi ya masharti ikiwemo suala la kumuongeza fedha za usajili na mshahara huku mazungumzo ya kurejeshwa Yacouba yakiendelea kufanyika.
Chanzo hicho kimesema kama mambo yataenda vizuri Yacouba atarejea ndani ya kikosi cha yanga kwa mkataba wa miaka miwili.
Aziz Ki anakadiriwa kupokea mshahara wa Tsh Milion 40, huku akitajwa kuwa ndiye mchezaji namba moja kuvuta mtonyo mrefu kuliko wote Ligi Kuu ya NBC.
Anafuatiwa na Clatous Chama ambaye amejiunga na Yanga akitokea Simba kwa dau la usajili Mil 800 TZS na mshahara wake unakadiriwa kufikia Tsh Milioni 35, akiwa nafasi ya pili kwa wanaolipwa pesa ndefu zaidi.