UONGOZI wa Simba umefanikiwa kunasa saini ya kiungo wa KMC FC, Awesu Awesu kwa mkataba wa miaka miwili baada ya makubaliano ya viongozi wa pande zote mbili.
Imeelezwa kuwa msimu ujao kiungo huyo ataonekana uwanjani akiwa na jezi ya rangi nyekundu na nyeupe kwa msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Bara na kombe la Shirikisho Afrika.
Usajili ya kiungo huyo ni kufikia mapendekezo ya benchi la ufundi ambalo lilipendekeza kusajili kwa mchezaji mzawa na Awesu ikiwa ni sehemu ya jicho la Wekundu hao wa Msimbazi.
Nyota huyo ambaye amekuwa akisifiwa na Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe alikiri kuwa katika viungo bora Awesu atakuwa kwenye orodha yake na angepewa nafasi ya kupendekeza usajili karata yake angeitupia kwa nyota huyo
Taarifa zilizopatikana kuwa uongozi wa Simba umefanikiwa kuzungumza na mchezaji huyo na kuwaeleza ana mkataba wa mwaka mmoja na kukaa meza moja na Waajiriwa wake walikubaliana kununua mkataba ulisalia.
“Ni kweli mazungumzo yalienda vizuri na Awesu ana mkataba wa mwaka mmoja ambao Simba wamekubali kuununua na kiungo huyo kuwa mali yao kwa msimu mpya wa mashindano,” alisema mtoa habari huyo.
Alipotafutwa mchezaji huyo alisema bado ana mkataba wa mwaka mmoja na KMC FC, wapo kwenye mazungumzo na Simba kwa ajili ya kutaka huduma yake.
“Simba wapo kwenye mazungumzo na KMC FC kwa sababu nina mkataba wa mwaka mmoja na Waajiriwa wangu hao ambao unaisha msimu wa 2024/25, kama mambo yakienda vizuri nipo tayari kuitumikia mpira ni kazi yangu,” amesema kiungo huyo.