AUCHO HAJATENDEWA HAKI, YANGA YAFUNGUKA ISHU YAKE, WAMEMUONEA
UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa ulitamani kiungo Khalid Aucho angekuwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo ya kiungo bora kutokana na kazi yake anayofanya ndani ya uwanja kitaifa na kimataifa.
Ipo wazi kwamba Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 walimaliza wakiwa na pointi 80 baada ya kucheza mechi 30 watapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni majina matatu yametajwa kuwania tuzo ya kiungo bora ni Aziz Ki wa Yanga, Feisal Salum na Kipre Junior hawa wote wanatoka Azam FC.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa wanatambua kuna vigezo ambavyo vimefuatwa lakini matamani ya Yanga ilikuwa ni kuona jina la kiungo Aucho linakuwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo hizo.
“Tungetamani zaidi mchezaji Khalid Aucho angejumuishwa kwenye category, kwa quality ya Aucho, kwa misimu aliyocheza sidhani kama kuna kiungo anaweza kumsogelea.
“Ila kama isingekuwa vigezo na namba ninaamini angekuwa anawania kiungo bora, MVP, kwenye kikosi bora Khalid ataingia.”
Usiku wa tuzo unatarajiwa kuwa Agosti Mosi, Masaki ambapo kitatangazwa pia kikosi bora cha msimu wa 2023/24.