TAARIFA kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) imeeleza kuwa timu tano Bongo zimefungiwa kufanya usajili wao kwa wakati huu mpaka zitakapokamilisha malipo ya wachezaji ambao wanawadai.
Kwenye orodha ya timu hizo tano mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 Yanga wamo pia katika orodha hiyo ambapo ili wafanye usajili jambo moja linatakiwa kukamilika haraka muda wowote kuanzia sasa ni malipo kisha watapewa ruhusa kufanya usajili.
Ipo wazi kwamba dirisha la usajili lilifungiliwa 15 2024 kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2024/25 kwa timu za Ligi Kuu Bara, Championship, First League na Ligi ya Wanawake Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) imeeleza namna hii: “Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezifungia klabu zifuatazo kusajili mpaka zitakapowalipa wachezaji wanaozidai.
“Yanga, Singida Fountain Gate FC, Tabora United FC, Biashara United FC na FGA Talents FC.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa klabu ambayo itawalipa wahusika, itaondolewa mara moja adhabu ya kufungiwa kusajili. Hadi leo asubuhi kupitia mfumo wa FIFA (FIFA legal portal) hakuna taarifa ya klabu yoyote kati ya hizo iliyowalipa wahusika.”