KONDE Boy ambaye alirejea kwa mara nyingine ndani ya Simba ni rasmi hatakuwa ndani ya kikosi hico akiungana na nyota wengine walioanza kukutana na Thank You.
Ni Luis Miquissone raia wa Msumbiji ambaye hakuwa na nafasi kikosi cha kwanza ndani ya Simba kitaifa na kimataifa Juni 19 2024 rasmi uongozi wa Simba ulibainisha kwamba hataongezewa mkataba kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Ikumbukwe kwamba zama alipokuwa ndani ya Simba mkali huyo alikuwa kwenye ubora wake na aliwapa tabu Waarabu wa Misri, Al Ahly kwa kuwafunga moja ya bao zuri kwenye mchezo wa Ligi ya MabingwaAfrika hali iliyopelekea wakampa dili la kupata changamoto mpya.
Alikwama kuonyesha ubora wake ndani ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo alitolewa kwa mkopo akitumia muda mwingi nje ya uwanja mpaka Simba walipomrejesha kwa mara nyingine tena.
Baada ya kurejea msimu wa 2023/24 ni mechi 19 kwenye NBC Premier League alicheza akitumia dakika 410 na kutoa pasi tatu zilizoleta mabao.
Rekodi zinaonyesha kuwa Miquissone amefunga bao moja katika mechi mbili alizocheza akiwa na jumla ya dakika 82 kwenye CRDB Federation Cup.