VITA ile iliyokuwa ikisaka mshindi mmoja ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023/24 imebaki gumzo baada ya kugota mwisho na mshindi kupatikana.
Kwenye mechi 30 ambazo ni dakika 2,700 kila kona walikamatana jambo ambalo liliongeza ushindani ndani ya uwanja kwa wababe hao wawili Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu Yusuph Dabo na Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda.
Ipo wazi kuwa awali ilikuwa kama utani lakini mwisho ikawa vita kweli kwa wababe hao wawili kusaka tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mabingwa Yanga walikuwa wakitazama nani atakuwa nani.
Azam FC mchezo wa mwisho walifunga kazi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold na Simba ilifunga kazi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania.Pointi wote ni 69 huku safu ya ushambuliaji ya Azam FC ikifunga mabao 61 ile ya Simba mabao 57.
Ukuta wa Azam FC uliruhusu mabao 21 na ule wa Simba ni mabao 25 uliruhusu hivyo kipande cha mabao ya kufunga na kufungwa kimewatenganisha Simba na nafasi ya pili ambapo watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika na Azam FC itakuwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika.
Funga kazi ilikuwa ni Mei 28 2024 ambapo kila kitu kilifahamika na Juni 2 2024 bingwa mpya wa CRDB Federation alifahamika ambaye ni Yanga kwa mara nyingine tena.
Ni msimu wa 2023/24 Simba imeporomoka kutokana nafasi ya pili iliyogotea msimu wa 2022/23 na Azam FC wamepanda kutoka nafasi ya tatu mpaka ya nne huku Yanga wakibaki palepale nafasi ya kwanza.