Mabao mawili ya dakika za majeruhi yaliyofungwa na Mato Joselu yalitosha kwa Real Madrid kupindua meza na kuichapa Bayern Munich mabao 2-1 na kutinga kibabe fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Awali ilionekana kama inakwenda kutokea fainali ya mwaka 2013 iliyokutanisha Bayern na Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Wembley.
Na hapo ingekuwa uwanja ni uleule na wababe ni walewale. Lakini, Bayern imeshindwa kulinda bao lake lililofungwa na Alphonso Davies baada ya kuruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili dakika 89 na 91 na straika Joselu na hivyo kupata tiketi ya kwenda kuchuana na Dortmund kwenye fainali itakayopigwa Wembley, Juni Mosi.
Chama hilo la Los Blancos limetinga fainali kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya sare ya 2-2 uwanjani Allianz Arena, Jumanne iliyopita.
Safari hii, mashabiki wamekosa fursa ya kuona marudio ya fainali ya mwaka 2013. Katika msimu huyo wa 2012-13, Bayern Munich ilikipiga na Borussia Dortmund katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa uwanjani Wembley na Bavaria iliibuka na ushindi wa 2-1, shukrani kwa mabao ya Mario Mandzukic na Arjen Robben, wakati bao la kujifariji la Dortmund lilifungwa na kiungo Ilkay Gundogan.
Na sasa ni kipute cha Dortmund na Real Madrid. Kipigo hicho kwa Bayern kinafanya timu hiyo ya Thomas Tuchel kumaliza msimu huu mikono mitupu, bila taji lolote ikiwa ni msimu wa kwanza kwa straika Harry Kane katika kikosi hicho cha Allianz Arena.
Ushindi huo umeibua ndoto za Los Blancos kuongeza taji la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiwa imebeba taji la La Liga msimu huu.
Dortmund yenyewe imetinga fainali baada ya kuisukuma nje Paris Saint-Germain kwa jumla ya mabao 2-0.
Fainali ya Ligiya Mabingwa Ulaya msimu huu itafanyika uwanjani Wembley, Juni Mosi. Patachimbika wakati mashabiki watakaposhuhudia wa Bundesliga watakapoonyesha kazi na wakali wa La Liga. Kazi ipo.