KLABU ya Yanga imefungiwa kusajili mpaka itakapomlipa aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo Lazarus Kambole.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeeleza kuwa uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu, (FIFA) baada ya mchezaji huyo kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.
Yanga ilitakiwa iwe imemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa lakini haikutekeleza hukumu hiyo.
Wakati FIFA imeifungia Yanga kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, TFF imeifungia kufanya uhamisho wa ndani.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF Cliford Ndimbo imeeleza kuwa TFF inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo imeingia na wachezaji pamoja na makocha kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.