Mabosi wa Yanga wameweka bayana msimamo wao wa kutaka kukata rufaa juu ya kulalamikia bao la kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz KI lililokataliwa jana katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini kigogo wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Aden Rage amefunguka juu ya rufaa hiyo.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Simba aliyewaji kuwa Katibu Mkuu wa TFF (enzi za FAT) amesema licha ya Yanga kudai iko tayari kukata rufaa katika Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kulalamikia bao hilo la Aziz KI, bado maamuzi ya mchezo huo hayatabadilishwa zaidi ya mwamuzi wa mchezo kuadhibiwa.
Yanga ilionekana kupata bao katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Luftus Versfeld, jijini Pretoria, Afrika Kusini dakika ya 59 alipofyatua shuti kali lililotokana na pasi ya Kennedy Musonda na kugonga besela kabla ya kuangukia ndani na kurudi tena uwanjani na VAR ikalikataa sio bao.
Kitendo cha kukataliwa kwa bao hilo kulifanya mchezo huo kumalizika kwa dakika 90 bila kufungana na kuamuliwa kupigwa kwa penalti na wenyeji Mamelodi ikapata ushindi wa 3-2 baada ya Aziz KI, Dickson Job na Ibrahim Bacca kila mmoja kukosa mkwaju wake na Yanga kung’oka michuanoni.
Kutokana na hali hiyo, mabosi wa Yanga ambayo inatarajiwa kuwasili nchini saa 2:10 usiku wa leo, imepanga kuwasilisha malalamiko yao CAF juu kitendo cha mwamuzi Dahane Beida wa Mauritania na wale wa VA kulikaa bao hilo lililoonekana halali kulingana na marejeo ya runinga.
Meneja Habari na Mawasiliano Yanga, Ally Kamwe alikaririwa jana kuwa wanamshukuru Mungu na wachezaji wao kwa ujumla kwa kila kilichotokea katika mchezo wao dhidi ya Mamelodi na kwamba kwa sasa kilichobakia ni kuendelea na michuano mingine iliyosalia ikiwemo ligi na FA ili kutokosa yote.
“Kuhusu swala lililotokea uwanjani, tutachukua hatua za kuwasiliana na CAF ili tupate muafaka lakini michuano hii imetufanya kuona ubora wa kikosi tulichonacho, lakini mechi hiyo ilisubiriwa kwa shauku kubwa na Afrika kwa jumla,” amesema Kamwe.
Hata hivyo, Rage amesema hata kama Yanga itaenda CAF matokeo yatabaki yalivyo ila ikitokea wakijiridhisha waamuzi wa mchezo huo walifanya makosa kitakachofanyika ni kuwaathibu kutokana na kanuni na sheria zao walizojiwekea.
“Mwenye maamuzi ya mwisho ni mwamuzi, hivyo hata akikataa bao la halali msimamo wake utaendelea kubaki kama ilivyo na baada tu ya hapo wahusika watakaa chini na kuangalia kilichotokea na kutolea maamuzi, lakini sio kubadili matokeo ya uwanjani.”
Rage amefafanua kuwa, utata uliojitokeza kwa bao hilo la Aziz KI ni kutokana na kutoonekana vizuri mpira wakati ukiwa ndani kwa sababu kwa pembe moja inaonyesha ni kweli uliingia, ila kwa kuangalia kamera za upande wa goli ni ngumu kujua uliingia au laah!.
Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi imeandika rekodi mpya baada ya kutinga hatua hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika histori ya timu hiyo tangu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika 1997.
Kwa mara ya kwanza Yanga iliwahi kucheza robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 ila tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu uliopita kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018 huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.
Timu hii ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi D kwa msimu huu ikiwa na pointi nane sawa na CR Belouizdad ya Algeria ila Yanga ilinufaika tu na faida ya jinsi zilivyokutana zikiwa nyuma ya mabingwa mara 11 wa michuano hiyo, Al Ahly iliyomaliza na pointi 12.