KIMATAIFA

INASIKITISHA: SABABU YA BEKI WA KAIZER CHEIFS KUPIGWA RISASI

Beki wa timu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini, Luke Fleurs [24] amefariki Dunia baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana huko jijini Johannesburg.

Nini kilichonyuma ya tukio hili la Luke Fleurs?

Tukio hilo la kupigwa Risasi limefanyika katika kituo cha mafuta usiku wa kuamkia leo katika kitongoji cha Johannesburg, Florida.

Nyota huyo wa Kaizer Chiefs mwenye umri wa miaka 24 alikuwa akisubiri kuhudumiwa na ndipo alipofikiwa na watu wasiojulikana wenye silaha na kumwamuru ashuke kwenye gari.

Mmoja wa washukiwa hao anaripotiwa kutoroka eneo la tukio na gari la Fleurs baada ya kumpiga risasi risasi.

“Washukiwa walimnyooshea bunduki na kumtoa nje ya gari lake, kisha wakampiga risasi moja kwenye sehemu ya juu ya mwili,” msemaji wa polisi wa Gauteng, Luteni Kanali Mavela Masondo aliambia vyombo vya habari vya ndani.

Kaizer Chiefs, moja ya vilabu maarufu nchini na mabingwa mara 12 wa ligi, imeeleza kuwa kifo chake kuwa cha kusikitisha, Klabu hiyo ilisema polisi wanashughulikia suala hilo na taarifa zaidi zitawasilishwa kwa wakati unaofaa.

Waziri wa Michezo Zizi Kodwa alisema “amehudhunishwa na kwamba maisha ya mwengine yamekatizwa kutokana na uhalifu wa kutumia nguvu”.

Historia Fupi ya Luke Fleurs.

Beki Fleurs alijiunga na Kaizer Chiefs mwaka jana, akiwa amewahi kuichezea SuperSport United.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa timu ya Under-23 aliiwakilisha Afrika Kusini kwenye Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mnamo 2021.

Alikuwa bado hajaichezea timu ya taifa ya wakubwa lakini aliripotiwa kukaribia kucheza mechi yake ya kwanza.

Katika tovuti yao, Kaizer Chiefs wanamtaja Fleurs kama “beki wa kiwango cha juu” mwenye “uwezo mkubwa wa kiufundi”.

“Asubuhi tumepokea habazi za kusikitisha na za kuhuzunisha za kufariki kijana wa kipekee ambaye bado alikuwa na wakati wa kuipambania ndoto yake,” Rais wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini Danny Jordaan alisema katika taarifa yake.

“Hii ni hasara kubwa kwa familia yake, marafiki, wachezaji wenzake na mpira wa miguu kwa ujumla.”

Mashabiki wa soka wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumuomboleza.

“Familia ya soka imepoteza mwali mkali,” mtangazaji wa soka Carol Tshabalala alichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Afrika Kusini inakabiliwa na ongezeko la matukio ya ufyatuaji risasi, huku matukio kadhaa ya risasi yakiripotiwa katika miaka ya hivi karibuni humo. Nchi hiyo ina moja ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, kulingana na data ya polisi.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button