Familia ya marehemu rapa Tupac ipo kwenye mpango wa kumfungulia mashitaka mwanamuziki Drake baada ya kutumia AI (akili bandia)kutengeneza sauti ya Tupac katika ngoma yake aliyokuwa akimchana Kendrick Lamar.
Kwa mujibu wa mwakilishi wa familia ya Tupac, Howard King ameripotiwa kutuma barua kwa Drake afute wimbo huo ndani ya saa 24 endapo hatafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Siku tano zilizopita Drake aliachia ngoma iitwayo ‘ Taylor Made Freestyle’ ambapo alitumia AI kutengeneza sauti ya marehemu Tupac na Snoop Dogg, ngoma ambayo ameitoa ikiwa ni dongo kwenda kwa Lamar wimbo huo ukiwa kama ni muendelezo wa bifu lao.
Bifu la wawili hao lilianza wiki chache zilizopita baada ya Drake kutoa ngoma iitwayo ‘First Person Shooter’ aliyomshirikisha Cole na kujinasibu kuwa wao ndiyo Big Three ya Rap wa kizazi hiki, jambo ambalo Kendrick Lamar hakupendezwa nalo na kuwajibu Drake na Cole.
Ikumbukwe kuwa Tupac alizaliwa Juni 16, 1971 na alifariki Septemba 13, 1996 akiwa na miaka 25, huku kesi ya mauaji ya kifo chake bado inaendelea