Wawakilishi wengine wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga, leo wanatupa karata yao katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwaalika Mabingwa wa Afrika Kusini Mamelodi Sundowns.
Mamelodi ni Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016 na ni moja ya timu zenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani humu.
Msimu uliopita wababe hao wa soka la Afrika Kusini waliishia hatua ya nusu fainali walipoondoshwa na Wydad Casablanca ya Morocco kwa kanuni ya goli la ugenini na msimu huu dhamira yao ni kuvuka kizingiti hicho.
Masandawana ni mabingwa watetezi wa michuano mipya ya African Football League (AFL).
Mchezo huo wa leo umevuta hisia za wapenda soka wengi Afrika kutokana na uzito wa majina ya timu zote mbili, Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu aliopita wakipoteza kwa kanuni ya goli la ugenini na msimu huu wamerudi kivingine kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Makocha wa timu zote mbili Miguel Gamondi wa Yanga ,na Rhulani Mokwena wa Sundowns wanafahamiana vizuri kwani kocha Gamondi amewahi kukinoa kikosi cha Masandawana hivyo kufahamiana kwao kunachochea msisimuko katika mchezo wa leo usiku.
Moja ya ukurasa unaotamaniwa kusomwa zaidi kwenye kitabu kitakachoandikwa baada ya mchezo huo ni eneo la golikipa ambapo makipa wawili bora kwa sasa Afrika watapigania nembo za timu zao ambapo Djigui Diarra ataiwakilisha Yanga wakati Ronwen Williams akiipigania nembo ya Masandawana.
Eneo la kiungo ni burudani pia kwa machizi soka wote kwani timu zote mbili zimesheheni viungo maridadi, wenyewe wamepewa majina ya mafundi wa gozi la N’gombe, huku kuna Mokoena, kule kuna Pacome, pale atakuwa Themba Zwane huku atakuwa Azizi Kii.
Saa tatu usiku ndio muda unaosubiriwa kumaliza ubishi wa miamba hawa miwili wa soka kwa sasa Afrika