MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Ally Mangungu amekanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni hivi karibuni kuwa klabu hiyo imenunuliwa na mwekezaji Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.
Mangungu amesema hayo baada ya kipande cha video kusambaa mitandaoni kikimuonesha Mo Dewji akihojiwa na kueleza kuwa ameinunua Simba kwa dola milioni 20 (zaidi ya Tsh bilioni 51), jambo ambalo liliibua taharuki na maswali yasiyo na majibu miongponi mwa mashabiki wa klabu hiyo na wadau wa soka nchini.
Akihojiwa na EFM, leo Jumatano, Machi 6, 2024, Mangungu amesema kuwa yeye si sehemu ya Mo Dewji hivyo hawezi kufafanua jambo ambalo hajazungumza yeye hivyo atasimama upande wa wanachama ambao yeye anauwakilisha ndani ya Simba.
“Hayo yanayosemwa na mimi nimeyasikia, nadhani kuna mapugufu kidogo kweye tafsiri ya maelezo ambayo yametolewa na wahusika. Mimi siwezi kuhusika kumjibia kwenye yale aliyoyasema kwa sababu mimi sio sehemu yake.
“Ninyi waandishi mnapenda kukimbilia kuwauliza watu mambo yaliyosemwa na watu wengine. Kama yeye ndiye aliyetoa hiyo kauli, sikutegema kama mimi ndiye nije studio kufafanua maelezo aliyoyatoa yeye, ilitakiwa ninyi mumuulize yeye. Simba haijawahi kuuzwa, haitokuja kuuzwa, Simba SC ipo.
“Kilichojitokeza ni uelewa wa watu wengi hata wanasimba wenyewe kuhusu mabadiliko yaliyofanyika ndani ya Simba. Mo Dewji ni mmoja wa watu waliojitolea sana kuisaidia Simba kwenye kipindi ambacho hakuwa sehemu ya Simba.
“Baada ya kujitoa sana, akatoa wazo kwamba tutengeneze mfumo ambao utasaidia watu kuwekeza ili klabu iwe ya ushindani zaidi. Ndipo tukaunda Simba Sports Club Company ambayo imegawanywa katika muundo wa share ya 51% kwa 49% ambayo iliwekwa na Serikali ili kuhakikisha kuwa wanachama wanakuwa majority shareholders.
“Simba imetoa mali zake na nguvu zake kuwekeza na mwekezaji ametoa pesa zake zikaunganishwa pamoja kutengeneza mtaji ili kuendesha klabu, huo ndiyo ukweli uliopo. Mchakato huo sasa upo hatua za mwisho,” amesema Mangungu.