Yanga iko zake kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kukusanya alama 40 katika mechi 15 ilizocheza ikiwa katika harakati za kutetea taji la Ligi Kuu Bara, huku beki wake Muivory Coast, Kouassi Attohoula Yao (27) akianza kunusa ufalme mapema.
Yao anayecheza eneo la beki wa kulia kabla ya mechi za juzi alikuwa kinara wa kutoa pasi za magoli ‘asisti’ akifanya hivyo mara sita sawa na winga wa Azam FC, Kipre Junior.
Huenda msimu huu ukawa wa kifalme kwa Yao kutokana na rekodi za asisti zilivyo katika misimu mitatu iliyopita kwa wachezaji wanaocheza eneo la ulinzi, yaani mabeki.
Katika misimu minne iliyopita kwenye Ligi Kuu Bara ni beki mmoja tu, Shomari Kapombe aliyekuwa akimiliki ufalme huo kwani ametoa asisti kuanzia tatu na kuendelea kwenye kila msimu.
Hata hivyo, Kapombe ndiye beki aliyetoa asisti nyingi zaidi kwenye msimu mmoja. Ilikuwa msimu uliopita wa 2022/2023 alipotoa asisti nane.
Katika msimu huo, Kiungo Mzambia wa Simba, Clatous Chama ndiye alikuwa kinara wa Asisti akitoa 14 akifuatiwa na Saidi Ntibanzonkiza aliyetoa 10.
Kapombe alikuwa beki mwenye asisti nyingi akiwa nazo nane akifuatiwa na Mohamed Hussein wa Simba aliyefanya hivyo mara sita.
Tayari Yao, amemfikia Hussein na sasa anaitafuta rekodi ya Kapombe ikiwa amebakiza mechi 15 za ligi jambo ambalo akiendelea na kiwango chake cha sasa ana nafasi kubwa ya kuzifikia na hata kuzidi na kujitengenezea ufalme wake.
Ukichukua asisti za Yao kwa msimu huu ukazipeleka msimu wa 2021/2022, basi angekuwa kinara wa kupiga pasi za mwisho katika msimu huo.
2021/2022 ulikuwa msimu mgumu kwa wakali wa Asisti kwani walioongoza walikuwa nazo sita pekee. Ni Abdulhaman Mussa wakati huo akiwa Ruvu Shooting na Reliants Lusajo aliyekuwa Namungo. Waliibuka vinara baada ya kila mmoja kupiga asisti sita. Kwa sasa wawili hao wote wako Mashujaa FC.
Aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Djuma Shaban ndiye aliongoza kwa mabeki waliotoa asisti nyingi msimu huo akitoa tano ambazo tayari Yao amezipita.

Beki mwingine aliyeingia kwenye orodha hiyo alikuwa Aboubakar Ngalema wa Dodoma Jiji aliyetoa nne huku Kapombe akiingia pia baada ya kumaliza msimu na asisti tatu sawa na Lusajo Mwaikenda (Azam) na Bruce Kangwa aliyeondoka Azam. Kiufupi kwa msimu huu hakuna beki aliyemfikia Yao wa sasa kwa Asisti.
Msimu wa 2020/2021 Kapombe aliibuka tena kama beki mwenye asisti nyingi. Hapa alitoa pasi za mabao saba sawa na nahodha wa Kagera Sugar, David Luhende.
Msimu huo Chama ndiye alikuwa kinara wa asisti akiwa nazo 15, alifuatiwa na Luis Miquissone (Simba), aliyetoa pasi za mabao 10 huku Rajabu Athuman aliyekuwa Gwambina na Idi Seleman ‘Nado’ wa Azam wakifuatia na asisti tisa.
Yao amebakiza asisti moja tu kuvunja rekodi ya mabeki Kapombe na Luhende kwa msimu huo. Yanga ina mechi 15 mkononi ambazo kama staa huyo aliyesajiliwa msimu huu asipoumia basi anaweza kutoa asisti zaidi na kupita saba za msimu huo.
Nafasi ya Yao kikosini kwa Yanga sio ya kusuasua kwani hata mshindani wake wa namba, Shomari Kibwana alithubutu kukiri ubora wa mkali huyo na kusema “Kazini kwangu kuna kazi.”
Kiufupi ukiachana na maamuzi ya benchi la ufundi kumpumzisha basi majeraha ndiyo yanaweza kumfanya Yao asivunje rekodi za mabeki kutoa asisti katika misimu mitatu iliyopita.
Hata hivyo msimu huu ni wa moto katika eneo hilo kwani licha ya Yao kuongoza kwa Asisti akiwa nazo sita, anafukuziwa kwa karibu na mabeki wengine, ambapo kabla ya mechi za jana Kapombe, Pascal Msindo na Mwaikenda wa Azam walikuwa nazo nne.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ anasema Yao ana nafasi kubwa ya kuendelea kutoa pasi za mabao kutokana na aina ya mfumo inayotumia Yanga. “Yanga ikiwa na mpira mara nyingi mabeki wa pembeni wanakuwa juu ya mstari wa kati hivyo wanatumika moja kwa moja kwenye kujenga mashambulizi.
“Yao ataendelea kutoa asisti kwani mfumo huo unambeba lakini pia ubora wake ni wa juu,” anasema Mwaisabula.
Mchambuzi wa soka wa gazeti la Mwanaspoti, Edo Kumwembe anasema Yao ana kipaji kikubwa na pia anajituma sana, hivyo hatashangaa kumuona akiendelea kutoa asisti.
“Yao ni mchezaji mzuri. Ana nguvu na ari ya kupambana wakati wowote. Pale Yanga ilipata beki na nadhani ataendelea kufanya makubwa kama hatapata majeraha,” alisema Edo.