Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini ‘TPBRC’ George Silas amesema ili pambano kati ya Hassan Mwakinyo na Twaha Kassimu ‘Kiduku’ lifanyike lazima mmoja kati ya mabondia hao afuate uzito wa mwingine.
Amesema Mwakinyo na Kiduku ni mabondia wanaocheza uzito tofauti lazima Watanzania wafahamu hilo, Twaha anacheza Super Middle Kilo 76 wakati Mwakinyo anacheza Super Welter Kilo 69.
“Hivyo kama kamisheni ya ngumi za kulipwa hatuwezi kuruhusu pambano ambalo mabondia wanaocheza uzito tofauti wapande ulingoni bila kuzingatia vigezo.”
“Mabondia wanapambana wakiwa na uzito sawa sio uzito tofauti, aidha kama Mwakinyo ana Kilo 69 anatakiwa kupambana na Twaha anapaswa kupanda uzito au kama Twaha anataka pambano na Mwakinyo ashuke,” amesema Silas.
Amesema ni pambano zuri ambalo kila mpenda mchezo wa masumbwi anatamani kulishuhudia na mwisho wa siku lazima mbabe ajulikane.
“Mimi niwaombe mapromota wa ngumi wawekeze kwenye hili pambano kwani ni kubwa na sisi kama kamisheni shauku yetu ni kuona mapambano yanafanyika na mchezo wa ngumi unaendelea kukua,” amesema Silas