MAMIA ya mashabiki wa soka nchini Ghana wameingia mitaani katika mji mkuu wa nchi hiyo Accra wakitaka utawala bora wa soka ujiuzulu, baada ya timu yao kushindwa kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).
Mashabiki hao walivaa fulana nyeusi na nyekundu wakisema “Okoa kandanda ya Ghana” wakiwa wameshikilia mabango, waliandamana katika barabara kuu kuonesha kufadhaika kwao kutokana na soka bovu la ‘Black Stars’.
Ghana, mabingwa mara nne wa Kombe la Mataifa ya Afrika, wamefuzu kwa Kombe la Dunia mara nne na kufika robo fainali mnamo 2010.
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ghana (GFA) lilimfuta kazi kocha Chris Hughton mwezi uliopita, baada ya timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu katika Kundi B kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika kwa pointi mbili katika mechi tatu.
GFA, inayoongozwa na Kurt Okraku, sasa itaajiri kocha wake wa tano wa Blacks Stars katika kipindi cha miaka mitano.