Unaweza kujiuliza maswali mengi baada ya kumuona kiungo mshambuliaji wa Yanga, Augustine Okrah ‘Magic’ akiwa amevaa kinyago kama cha straika Victor Osmhen wa Napoli ambaye kwa sasa yupo zake Ivory Coast akiitumikia timu yake ya Taifa ya Nigeria katika fainali za Afcon.
‘Mask’ ya Osimhen anayopenda kuivaa kila mara uwanjani ilitokana na mazoea aliyojijengea baada ya kupona sehemu ya fuvu iliyopata ufa wakati flani. Nyota mwingine aliyezoeleweka kuvaa kwa staili hiyo enzi zake alikuwa staa wa zamani wa Uholanzi, Edgar Davis aliyecheza Juventus, Barcelona, AC Milan, Tottenham Hotspur, Inter Milan na Crystal Palace.
Ipo hivi. Okrah alisajiliwa dirisha dogo la usajili wakati Yanga ipo katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, na alitambulishwa kwa staili flani hivi kama mazingaombwe kutokana na jina lake la a.k.a Magic, na hukohuko Zanzibar alicheza mechi ya kwanza Yanga kwa dakika kumi katika mchezo dhidi ya KVZ katika mashindano hayo
Baada ya kutoonekana kwenye mechi za kwanza ya Ligi Kuu Bara baada ya mapumziko ya Afcon, Yanga ikicheza dhidi ya Hausung kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na pia dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Ligi Kuu, ukimya ulitawala juu ya nyota huyo wa kimataifa wa Ghana iwapo alikuwa amepona au la.
Hata hivyo, kutoonekana kwake kulijibiwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe aliyesema Okrah anauguza majeraha, lakini ataonekana uwanjani muda sio mrefu akiwa amevaa ‘mask’.
“Ni kweli Okrah hajaonekana. Bado anauguza majeraha lakini muda si mrefu ataonekana uwanjani tena akiwa amevaa mask kama Osmhen kutokana na jeraha alilolipata katika maneno ya uso,” alisema Kamwe.