Rais wa Chama cha Soka Cameroon (Fecafoot), Samuel Eto’o ambaye ni mchezaji wa zamani pia wa Taifa hilo ametuhumiwa kuhusika na masuala ya upangaji wa matokeo na kutoa vitisho nchini humo.
Kwaa mujibu wa gazeti la The Athletic faili la Eto’o linachunguzwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lakini pia limeshawasilishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA) na Makamu wa rais wa zamani wa Fecafoot, Henry Njalla Quan
Eto’o anakabiliwa na orodha kubwa ya tuhuma nyingi ikiwemo upangaji matokeo, kusambaza taarifa za uongo, kutoa vitisho, kusababisha vurugu na matumizi mabaya ya ofisi.
CAF pia imethibitisha kuwa inachunguza kuhusiana na madai hayo dhidi ya Eto’o na FIFA iliwahi kushauriwa kumtoa staa huyo wa zamani wa Barcelona katika nafasi yake kutokana na mfululizo wa matukio tata.
Njalla Quan Junior amedai kwamba mechi kati ya akademi yake na Kumba City FC ilipangwa matokeo na Eto’o, akieleza tukio hilo kama moja ya “kashfa kubwa kabisa maishani”.
Pia Eto’o anatuhumiwa kupanga matokeo ya timu ya “rafiki yake wa karibu“ Valentine Nkwain ipande daraja. Victoria United ikapanda daraja baada ya kushinda mechi 11 kati ya 17 za mwisho wa msimu licha ya kupoteza mechi nne kati ya saba za kwanza za msimu huo.
Gazeti la The Athletic likaongeza kuwa uhusiano wa Njalla Quan Junior na Eto’o uliharibika kabisa na mshambuliaji huyo wa zamani kudaiwa kumlipa mtu atume meseji ya vitisho.
Ilisomeka: “Mimi ni mafia wa mapinduzi haya na katika umafia huu hatuwasaliti viongozi wetu. Nimekuwa nikilinda maslahi ya mipango yetu hadi leo. Hivyo kama utanizingua kaa tayari kubeba mzigo wa kitakachotokea.”