Yanga ipo kwenye maandalizi ya kuelekea Afrika Kusini kwaajili ya mchezo wa marudiano, Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ambapo taarifa njema ni kuwa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo itawagharamikia mashabiki 48 ambao wataenda Afrika Kusini.
Hayo yamesemwa na rais wa Yanga Eng Hersi Said katika mkutano siku ya leo.
“Tunafahamu Klabu yetu ya Young Africans SC ina mchezo mwingine wa pili kule Afrika Kusini hivyo Uongozi wenu umefanya jitihada za kupeleka Ombi katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wetu Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro la kusafirisha mashabiki kwa njia ya Basi na tunaishukuru Wizara kwa kukubali Ombi letu.
Wizara itahudumia gharama zote za safari ya kuelekea Afrika kusini yenye Wanachama na Mashabiki wetu 48 kuanzia Nauli mpaka pesa ya kujikimu, hivyo sisi Young Africans tunaishukuru sana Wizara.
Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na shilingi laki 6 na tulipata watu 30, niwahakikishie baada ya Wizara kukubali kusafirisha Wanachama na Mashabiki wetu,zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe.
Niwatakie safari njema na nina imani safari yetu ya kurudi itakuwa nzuri kwakuwa tutarudi tukiwa tayari tumeshafuzu hatua ya nusu Fainali” Rais wa Young Africans SC Eng. Hersi Said akiongea na Wanahabari wakati wa kuwaaga Wanachama na Mashabiki wanaosafiri kuelekea Afrika Kusini Makao Makuu ya Klabu Jangwani.