KISA KIBU: ROBERTINHO AMVAA UPYA BENCHIKHA
Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameshtuka kusikia taarifa kwamba straika wa Simba, Kibu Denis ‘Mkandaji’ kwa sasa hapati namba katika kikosi cha kwanza na kufichua huenda benchi la ufundi lililopo limeshindwa kumtumia vyema tofauti na alivyokuwa akimtumia yeye na kumfanya awe tishio.
Kocha huyo Mbrazili aliyetimuliwa na Simba mara baada ya Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana amesema amekuwa akifuatilia taarifa juu ya kikosi hicho na hasa Kibu, mmoja ya wachezaji aliokuwa wakiwapenda na kuwatumia katika kikosi chake cha kwanza na kujua ameporomoka vibaya.
Robertinho alisema kwa mtazamo wake anadhani Simba wanakosea kumtumia Kibu na huenda wanashindwa kumsaidia kama alivyomsaidi yeye kipindi akiwa Msimbazi.
Robertinho alisema alikuwa anajua namna ya kuishi na Kibu kwa kuzungumza naye kila wakati na kumpa majukumu ya kimkakati aliyokuwa akiyatekeleza vizuri uwanjani na kumfanya awe mmoja ya wachezaji wanaogopwa na wapinzani.
Alifafanua kwa kusema, ana wasiwasi kuhusu mshambuliaji huyo amekuwa akiishi maisha ya kuogopa makocha nyuma yake baada ya kuondoka, jambo ambalo Benchikha na wenzake wanatakiwa kukaa na kuzungumza naye kwa kina.
“Nikweli naona hajafanyi vizuri sana, ingawa hata nilipokuwa naye hakufunga sana lakini alikuwa na msaada mkubwa kwa timu pengine kuliko kufunga. Kibu hataki mambo ya ukali sio kila binadamu anaweza kuhimili hilo, nililigundua nilipokuwa naye, nikatafuta namna ya kuishi naye kwa kuwa na kuanza kujenga urafiki na kuzungumza naye kwa ukaribu,” alisema kocha huyo na kuongeza;
“Ukiacha viungo wakabaji hakuna kiungo mwingine anaweza kukupa kazi bora kama Kibu, kama utampa mikakati ya kuifanya uwanjani akabaje na wakati gani ashambulie nini na awe mtulivu
“Sikujali kukosea kwake nilijali ufanisi wa niliyompa ayafanye uwanjani hata kama mashabiki walikuwa hawavutiwi naye kuna mambo kwangu kama kocha alisaidia zaidi kuliko kufunga.”
Aidha kocha huyo aliyetuimuliwa Simba akiwa na rekodi ya kupoteza mechi moja tu ya Ligi Kuu aliyoiongoza timu katika mechi 17 na kushinda 14 na sare mbuili akifunga mabao 42 na kuruhusu 15 kwa muda wote aliokuwapo tangu alipoajiriwa Januari mwaka jana, alizungumzia pambano lijalo la Simba na Al Ahly akisema kama atarejeshewa utulivu na kisha kupangwa Kibu huenda akawasaidia.
“Unakumbuka tulipocheza na Ahly hapo na kule kwao? Kumbuka kazi ambayo Kibu alifanya ile ilitokana na kukaa naye na kupanga mikakati, kama angekuwa sawa hizi mechi angeisaidia sana Simba kwa kuwa ni mchezaji aliyechagua kujituma kwa muda wote akiwa uwanjani,” alisema Robertinho.