PAMOJA NA KUFURUSHWA YANGA…GAMONDI KASALIA BONGO….HUENDA AKATUA TIMU HII
BAADA ya klabu ya Singida Black Stars kumsimamisha kazi Kocha Mkuu, Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi ambao wote walishawahi pia kufanya kazi Simba SC, habari zinasema huenda kocha wa zamani wa Yanga, Miguel Gamondi akachukua mikoba ya kukinoa kikosi hicho.
Klabu hiyo jana ilitoa taarifa kupitia ofisa habari wake, Hussein Massanza kuwasimamisha makocha hao kwa kile ilichodai ni mwendo usioridhisha katika michezo mitatu mfululizo, licha ya jitihada zote kufanyika kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo kuwapatia benchi la ufundi kwa kila wanachohitaji.
Amesema kuwa maamuzi hayo yamefanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo iliyochaguliwa hivi karibuni.
“Kipindi chote ambacho Aussems na Kitambi hawatakuwa kazini, kikosi kitakuwa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Ramadhani Nsanzurwimo kama kocha mkuu, huku msaidizi wake akiwa Muhibu Kanu.
Massanza amesema, si kawaida ya timu yao kwa msimu huu kucheza michezo mitatu bila ushindi, kwao hawataki uzoeleke na usionekana wa kawaida kwani Singida pia ina kikosi bora kama timu zingine kubwa zinazowania ubingwa.
“Ukiangalia timu tunazotoa nazo sare ukazilinganisha na Singida Black Stars, tumezipita kiwango kwa kiasi kikubwa, kwa maana hii timu inaonesha inaanza dalili za kushuka kiwango, Bodi ya Wakurugenzi ikaona ichukue hatua hizi ambazo ni za mwanzo, huko mbele tutaangalia nini kitaendelea,” amesema.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema klabu hiyo imekuwa na mazungumzo na Gamondi aliyetimuliwa hivi karibuni na Yanga, ambaye bado yupo nchini.
Taarifa zinasema huenda akapewa mkataba wa miaka miwili na anaweza kutambulishwa wakati wowote ule mambo yatakapokamilika.
Akizungumzia hilo, Massanza amesema bado halijafika mezani kwake, analofahamu kwa sasa ni kwamba makocha hao wamesimamishwa, lakini chochote kikitokea ataujulisha umma.