KWA SIMBA HII, UBINGWA MSIMU HUU NI WA UHAKIKA
KWA misimu mitatu mfululizo, Simba imekuwa ikipishana na ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya watani wao, Yanga kubeba back to back, lakini kwa msimu huu Wekundu wa Msimbazi hao wameonyesha kiu ya kutaka kurejesha heshima iliyoipoteza.
Aina ya usajili uliofanywa sambamba na uboreshwaji wa benchi la ufundi ni mambo yanayoashiria kwamba msimu huu, Simba imekuja kivingine na hata kasi waliyoanza nayo katika mechi nane za awali wa Ligi Kuu Bara ni ishara hata wao ubingwa wanautaka.
Hata hivyo, haiwezi kuwa kazi rahisi kama Simba haitafunga buti vilivyo, kutokana na timu nyingine zilizopo katika ligi hiyo zilivyojipanga kuanzia watetezi, Yanga, Azam FC hadi Singida Black Stars iliyokuwa inaongoza msimamo kwa muda mrefu kabla ya kushushwa na Yanga.
Ukisikiliza kauli za viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa klabu hiyo, unaiona wazi mipango iliyonayo Simba msimu huu, jinsi wanavyotamani kuwapa kicheko wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kwa kubeba ubingwa, ingawa haiwezi kuwa rahisi kama haitaishi kwa hesabu kali.
Hapa chini kuna mambo matano ambayo kama Simba itakomaa nayo mwanzo mwisho na kutokubali kudondosha pointi zaidi, basi kuna kila sababu ya timu hiyo kurejesha taji hilo Msimbazi na kuwakatili watani wao Yanga wanaotaka kufikia rekodi wa Wekundu hao kubeba taji mara nne mfululizo.
Ndio, kabla ya Yanga kufanya mapinduzi, Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu minne mfululizo ikiwa ni rekodi kwa miaka ya karibuni, ikifanya hivyo 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021, lakini sasa ina nafasi ya kupindua meza sambamba na kubeba Kombe la Shirikisho (FA) ambalo kwa misimu mitatu pia haijalitia mkononi kutokana na kutawaliwa na watani wao hao wa Jangwani.
UCHEZAJI NA MBINU ZA UFUNDI
Simba ya Kocha Fadlu Davids imekuwa ikitumia mifumo ya 4-2-3-1 na 4-4-2 ambayo imeiwezesha wachezaji kunyumbulika, kufanya majukumu mengi uwanjani na hilo wamekiri kwa nyakati tofauti.
Aliwahi kusema hivyo mshambuliaji wa timu hiyo, Valentino Mashaka; “Kocha anapenda mchezaji anayeweza kujiongeza kufanya jukumu zaidi ya moja uwanjani, huwa anatuambia mchezaji wa kisasa lazima afanye hayo.”
Mwingine ni Edwin Balua amesema; “Siwezi kushangaa kocha akinipanga kucheza nafasi nje na ile niliyoizoea kwani anataka tuwe tunanyambulika na kusaidiana majukumu.”
Tukija kwa mifumo ya Fadlu: Inatoa uwiano mzuri kati ya kushambulia na kuzuia, huku ukihakikisha kuwa timu inashambulia kwa mpangilio mzuri lakini pia inalinda goli lao kwa umakini.
Uwezo wa Fadlu kuwatumia wachezaji kulingana na mfumo uliopo unaifanya Simba kuwa na mchezo unaoeleweka na unaoongeza ushindani dhidi ya wapinzani.
Pia, kwa kufundishwa mbinu za kisasa, wachezaji wamepata uwezo wa kuhimili mbinu tofauti za wapinzani wao, jambo linaloongeza uthabiti wa timu.
Uthabiti huu kwenye mfumo wa uchezaji unawapa wachezaji ujasiri wa kucheza kwa kushirikiana vizuri na kuelewa namna bora ya kudhibiti mchezo ili kuhakikisha timu inapata ushindi.
KUIMARIKA KWA KIKOSI
Pamoja na maigizo mapya Simba kama Leonel Ateba, Joshua Mutale na Jean Charles Ahoua, inahitaji muunganiko na uzoefu utakaofanya kila mechi iwe nyepesi kwao.
Data za wachezaji hao zinaonyesha walikotoka walifanya mambo makubwa mfano Mutale akiwa na Power Dynamos alifunga mabao manane, (Simba bado hajafunga, hana asisti), Steven Mukwala msimu uliopita akiwa na Asante Kotoko ya Ghana alifunga mabao 14 na kwa Wanamsimbazi hadi sasa ana bao moja na asisti moja.
Mchezaji ambaye angalau kajipambanua ni Ahoua ambaye kahusika katika asisti nne na kafunga mabao matatu, hivyo kahusika katika mabao saba na amekuwa faraja kwa mashabiki akiwa ndani ya uwanja wanajua kuna kitu atakionyesha.
Ukiachana na Ahoua, mshambuliaji mwingine Ateba ambaye akiwa USM Alger katika mechi 12 alifunga bao moja, lakini Simba tayari ametupia mawili na asisti mbili na uchezaji wake ni wa kutumia nguvu.
Kuna wale ambao viwango vyao bado havijaanza kuonyesha ushindani mfano kama Valentine Nouma ambaye ikitokea kaumia nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ au Abdulrazack Hamza linaonekana pengo.
Simba inaonekana bado inahitaji kuongeza nguvu zaidi katika kikosi, imemsajili Elie Mpanzu na bado kocha Fadlu alikiri katika moja ya mahojiano yake, usajili wa dirisha dogo wataongeza wachezaji.
“Tutaongeza nguvu katika maeneo machache kwa lengo la kuongeza makali zaidi ya kikosi chetu, tupo kwenye mwelekeo mzuri na naamini kila kitu kitakuwa sawa, nina furaha kuwa na kundi hili la vijana, kila mmoja anapambana.”
Rekodi zinaonyesha katika mechi nane za awali za Ligi Kuu msimu huu, Simba imefunga jumla ya mabao 16 na kuruhusu matatu tu, ikiwa ni wastani mzuri, ingawa tayari imeshadondosha pointi tano kutokana na sare ya 2-2 mbele ya Coastal Union na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga.
Ni wazi kwa mechi 22 ilizobakia nazo. Simba haipaswi kudondosha tena alama kama kweli inataka ubingwa kwani imeachwa pointi tano na wapinzani wao wa jadi, Yanga waliopo kileleni, pia Singida Black Stars wanaofuatia wakiwa na wastani mzuri katika mechi walizocheza.
MAANDALIZI NA NIDHAMU
Moja ya mambo muhimu yanayochangia mafanikio ya timu yoyote ni maandalizi thabiti na nidhamu. Benchi la ufundi la Simba linafanya kazi kubwa kuandaa wachezaji wao kimwili na kiakili ili wawe na nguvu na utayari wa kucheza mechi nyingi bila kuchoka.
Mazoezi ya viungo na yale ya mbinu huwasaidia wachezaji kuwa na stamina inayowawezesha kuhimili mikikimikiki ya ligi, hasa wakati wa kipindi kigumu cha mechi mfululizo.
Nidhamu ya wachezaji inaboresha utimamu wao na kuwafanya kuwa na uwajibikaji mkubwa. Wachezaji wanafuata ratiba za mazoezi, wanazingatia mlo sahihi na kujiepusha na majeraha yanayoweza kuathiri kiwango chao.
Vilevile, nidhamu inawahimiza wachezaji kushirikiana kwa karibu, kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, na kuheshimu malengo ya timu, jambo ambalo linaweza kupelekea mafanikio ya Simba msimu huu, nje na hapo itakuwa vigumu kutimiza kwa matendo ndoto zao.
MSETO WA KIKOSI
Simba imefanikiwa kuwa na mchanganyiko bora wa wachezaji wenye uzoefu na vijana wenye ari, jambo ambalo linaboresha ufanisi wa timu uwanjani.
Kwa upande wa uzoefu, wachezaji kama Shomary Kapombe na Mohammed Hussein wanaweza kuiongoza timu na kutoa ushauri kwa vijana. Wachezaji hawa wanajua nini kinachohitajika katika mechi ngumu na wana uwezo wa kuleta utulivu na uongozi wakati timu inakutana na changamoto uwanjani.
Vijana kama Edwin Balua, Mutale, Ahoua, kwa upande mwingine, wanachangia kasi na nguvu mpya inayosaidia timu kupambana dhidi ya wapinzani. Mchanganyiko huu unaleta uwiano wa mbinu na nguvu, hali inayosaidia timu kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za aina yoyote uwanjani.
Pia, inakuwa rahisi kwa timu kupata matokeo bora, kwani vijana wana hamu ya kuonyesha uwezo wao huku wakisaidiwa na uzoefu wa wakongwe.
UONGOZI NA SAPOTI YA MASHABIKI
Simba inafaidika na uongozi bora ambao unahakikisha timu inapata mahitaji muhimu, ikiwa ni pamoja na usajili, mafunzo na mazingira mazuri ya kazi kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Uongozi huu unawapa wachezaji hali ya kujiamini na utulivu, na hivyo kuwafanya waweze kujituma ipasavyo uwanjani.
Pia, viongozi wanahakikisha malengo ya timu yanasimamiwa ipasavyo ili kufikia matarajio ya mashabiki.
Mashabiki wa Simba wanaipa timu nguvu na motisha kwa kujitokeza kwa wingi na kushangilia, jambo ambalo linachangia hamasa kwa wachezaji.
Sapoti hii ni muhimu hasa katika mechi ngumu na sauti za mashabiki huwapa wachezaji ari na nguvu ya kushinda.
Mashabiki wa Simba wamekuwa nguzo muhimu kwa mafanikio ya timu hiyo na wanapokuwa nyuma ya timu, wachezaji wanapata motisha zaidi ya kupambana kwa ajili ya mashabiki wao na kuleta furaha katika klabu.
Kwa kuzingatia mambo haya matano uthabiti wa mfumo wa uchezaji, usajili bora, maandalizi thabiti, mchanganyiko wa uzoefu na vijana, na uongozi imara pamoja na sapoti ya mashabiki Simba SC inajiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Ikiwa timu itaendelea kufuata mipango yake na kuboresha maeneo yanayohitaji marekebisho, uwezekano wa kutimiza lengo lao la ubingwa mbele ya washindani wake, Yanga na Azam FC.
ALICHOSEMA GARINCHA
Staa wa zamani wa timu hiyo, Steven Mapunda ‘Garincha’ ushauri wake ni wachezaji kuongeza nguvu ya kujituma uwanjani, umakini na uzalendo kwa klabu, wakizingatia hayo anaona njia ya ubingwa kwao ipo wazi.
“Japo Simba imedondosha pointi tano kwa kufunga na Yanga bao 1-0 na kutoka sare ya mabao 2-2 na Coastal Union, haimanishi ubingwa wameupoteza, bado safari ni ndefu, hawapaswi kusikiliza maneno ya mashabiki, bali wapambane kwa bidii,” alisema Garincha huku kocha wa zamani wa Gwambina, Mtibwa Sugar na timu ya vijana Azam FC, Mohamed Badru akisema: “Simba inahitaji muunganiko, wachezaji waongeze kujiamini na umakini mkubwa, naamini bado wana nafasi ya kuchukua ubingwa, kwani wana kikosi kizuri.”
POINTI ILIZODONDOSHA
2024/25-Pointi 5
Simba 2-2 Coastal
Simba 0-1 Yanga
2023/24- Pointi 19
Simba 1-5 Yanga
Simba 1-1 Azam
KMC 2-2 Simba
Simba 1-2 TZ Prisons
Ihefu 1-1 Simba
Yanga 2-1 Simba
Namungo 2-2 Simba
Kagera 1-1 Simba
2022/23-Pointi 17
Simba 2-2 KMC
Mbeya City 1-1 Simba
Singida FG 1-1 Simba
Yanga1-1 Simba
Azam 1-0 Simba
Kagera 1-1 Simba
Simba 1-1 Azam
Namungo 1-1 Simba
2021/22- Pointi 29
Biashara Utd 0-0 Simba
Simba 0-0 Coastal
Simba 0-0 Yanga
Mbeya City 1-0 Simba
Mtibwa 0-0 Simba
Polisi TZ 0-0 Simba
Yanga 0-0 Simba
Namungo 2-2 Simba
Azam 1-1 Simba
Geita Gold 1-1 Simba
TZ Prisons 1-0 Simba
Kagera 1-0 Simba
Mbeya Kwanza 0-0 Simba
Credit:- MwanaSpoti