Beki wa kazi ndani ya kikosi cha Simba, Che Malone ameweka wazi kuwa matokeo yaliyopita kwenye Kariakoo Dabi hayawezi kubadilika hivyo wanachofanya ni maandalizi mazuri kuelekea mchezo ujao unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Ipo wazi kuwa msimu wa 2023/24 Simba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 1-5 Yanga na mchezo wa mzunguko wa pili ilikuwa Yanga 2-1 Simba.
Ndani ya dakika 180 Simba ilipoteza pointi tatu mazima na safu ya ulinzi iliokota nyavuni mabao 7 huku safu ya ushambuliaji ya Simba ikifunga mabao mawili moja likifungwa na Kibu Dennis kwa pasi ya Saido Ntibanzokiza mzunguko wa kwanza na moja likifungwa na Fred Michael kwa pasi ya Clatous Chama.
Beki huyo amesema: “Tunatambua tuna mchezo mkubwa ujao dhidi ya Yanga ambao ni muhimu kwetu kupata ushindi, matokeo yaliyopita yameshatokea na hatuwezi kuyabadili hivyo ni muhimu kufanyia kazi makosa yaliyopita kwenye mchezo ujao.
“Ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri hilo tunalitambua ambacho tunapaswa kufanya ni kushirikiana vizuri kwenye kila eneo kuwazuia wachezaji wao wazuri ndani ya uwanja.”