NYOTA wa Simba kiungo Edwin Balua aliyewazima wapinzani wao kwenye anga la kimataifa jioni amefichua alichoambiwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids kabla ya kuingia kwenye mchezo huo.
Septemba 22 2024 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 3-1 Al Ahli Tripoli huku mabao ya Simba yakifungwa na Kibu Denns dakika ya 36, Leonel Ateba dakika ya 45 na Balua dakika ya 89 muda mfupi baada ya Simba kufanyiwa shambulizi la hatari na mfungaji wa bao la kwanza kwa Tripoli Cristivo Mabululu.
Balua aliingia kwenye mchezo huo akitokea benchi alifunga bao lililowavuruga Waarabu hao wa Libya mpaka mpira unagota mwisho walikuwa wakilalamika jambo lililopelekea mwamuzi wa kati kumuonyesha kadi nyekundu mfungaji wa bao laTripoli Mabululu.
Kiungo huyo alifunga bao hilo kwa utulivu mkubwa ambapo alikuwa na nafasi ya kutoa pasi kwa wachezaji wawili wa Simba waliokuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga ikiwa ni pamoja na Ateba ila chaguo lake ilikuwa kufunga mwenyewe.
“Mwalimu anajua namna ya kuelekeza wachezaji na aina ya mchezo ambao tunacheza ambacho alisema ilikuwa anahitaji kuonatunapata ushindi hivyo nilivyoingia nilikuwa ninawaza ushindi hakuna kingine.
“Ukiwa umefungwa ama ukiwa unaongoza lakini kuna nafasi ya kufungwa hapo presha inakuwa kubwa lakini tulipofunga bao la tatu naona tulikuwa tumemaliza kabisa mchezo na ushindi ukawa kwetu, mashabiki tunawashukuru wamejitokeza kwa wingi.”