Haijamchukua Samatta hadi astaafu ndipo aheshimike. Juzi juzi tu tumecheza na Ethiopia na tayari umma wa Watanzania umemkumbuka. Mechi mbovu ya kawaida huku wachezaji wengi wa eneo la mbele wakishindwa kuonyesha makali yao, tayari Watanzania wamemkumbuka Samatta.
Huu ndio unafiki wa Watanzania katika ubora wake. Ukweli ni kwamba Samatta bado hayupo katika ubora wake lakini bado ana nafasi ya kuonyesha uzoefu wake uwanjani. Kama sio kwa mechi nzima basi ni kwa dakika kadhaa.
Kuwepo kwake uwanjani tu kunawafanya baadhi ya wachezaji wa timu pinzani kuwa na hofu naye. Hapo ndipo kina Simon Msuva wanafunga mabao na bado tunatoa kejeli kwa Samatta hajitumi uwanjani isipokuwa Msuva ndiye anayejituma zaidi.
Hata mwamuzi akimwona Samatta anaweka heshima zaidi kwake kwa sababu anajua wasifu wake. Ni kitu cha kawaida ndiyo maana imeletwa staili ya kumpa unahodha mchezaji ambaye ni staa zaidi katika taifa. Messi kwa Argentina, Ronaldo kwa Ureno, Neymar kwa Brazil, Mbappe kwa Ufaransa. Mifano ni mingi.
— Edo Kumwembe, Legend.