BAADA ya sintofahamu ya muda mrefu kuhusiana na usajili wa mchezaji, Lameck Lawi, imeamuliwa nyota huyo ataitumikia timu yake ya zamani, Coastal Union, imefahamika.
Lawi ambaye alikuwa anagombewa na Simba na Coastal Union, sasa ataonekana uwanjani Septemba 13, mwaka huu wakati Wagosi wa Kaya watakapoivaa Mashujaa FC.
Ofisa Habari wa Coastal Union, Abbas El Sabri, amesema baada ya mazungumzo na Simba, hatimaye wamefikia mwafaka wa mchezaji huyo kusalia kwao, hivyo tayari wamefunga rasmi sakata hilo.
“Suala la Lawi limekuwa na maswali mengi sana, lakini majibu yake yatapatikana Septemba 13, mwaka huu tutakapomtumia katika mchezo wetu dhidi ya Mashujaa FC, hapo tutakuwa tumejibu kila kitu tulichoulizwa, hili jambo limeshamalizika, huyu kwa sasa ni mchezaji halali wa Coastal Union,” alisema El Sabri.
Aliongeza walikaa vikao viwili baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji kuwataka kumalizana wenyewe na hatimaye wamefikia makubaliano mazuri.
“Ni kweli Simba wamekuwa waungwana, tumekaa nao vikao viwili na tumekubaliana, uungwana ndiyo unaotakiwa kwenye mpira, nasi pia tunawashukuru wenzetu, sisi pia tunaahidi tutafanya uungwana zaidi kwao, tunawashukuru sana,” aliongeza.
Wakati huo huo, Coastal Union, inatajwa huenda ikamchukua Kocha Mrundi Dominique Niyonzima, kwa ajili ya kurithi mikoba ya David Ouma, aliyetimuliwa.
El Sabri alikiri kuwa wapo katika mchakato wa mwisho kumtangaza kocha, lakini hatutakataa wala kukubali kumtwaa kocha huyo.
“Mpaka sasa tunakamilisha mchakato wa benchi la ufundi, ambalo tunaamini litatuvusha.
“Tumesikia tunahusishwa na Kocha Niyonzima, na sisi tunafurahi kwa sababu tunahusishwa na mmoja na makocha wakubwa kabisa katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati, sisi pia tuna ndoto ya kuwa na kocha kama huyo,” aliongeza.