Aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Freddy Michael ameshindwa kujiunga na USM Alger ya Algeria kwa kigezo cha kutowahi kuichezea timu ya taifa, lakini mwenyewe amezima uvumi kwamba yupo nchini akivizia dirisha dogo ili ajiunge na Yanga kuchukua nafasi ya Kennedy Musonda.
Inadaiwa, ili uweze kucheze soka la kulipwa Algeria ni lazima angalau umepita timu ya taifa japo ile ya vijana na Freddy hajawahi kufanya hivyo na kukwamisha dili la kusaini USM Alger na mchezaji huyo kuamua kurudi nchini na kuungana na mastaa wa Yanga aliokuwa akijifua nao na kuibua hisia za kutua huko.
Freddy alikwenda kukamilisha dili hilo la Algeria baada ya kuachana na Simba aliyoichezea nusu msimu na akafunga mabao sita ya Ligi Kuu, huku akiibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Zambia akifunga mabao 11 wakati akiwa na Green Eagle kabla ya kujua Msimbazi. Simba ilimtema hivi karibuni kumpisha Lionel Ateba kutoka klabu hiyo ya Algeria.
Baada ya dili hilo kufeli, Freddy amerejea Tanzania na kuliibuka tetesi nyingi, zikisema Yanga inamendea huduma yake, ili kumsajili kupitia usajili wa dirisha dogo, ikielezwa huenda itaachana na Musonda aliyecheza dakika 1116 alifunga mabao matano, asisti mbili kupitia mechi 22.
Suala la Musonda kuondoka Yanga aliyojiunga nayo tangu Januari, 2023 akitokea Power Dynamo ya Zambia ni la muda, kwani usajili uliopita aliponea chupuchupu kukatwa kikosi hicho, ambapo Simba ilikuwa inahusishwa kumhitaji.
“Musonda hayupo kwenye mipango ya kocha, alibaki kwa sababu ya kumpa nguvu Prince Dube, lakini baada ya kufanikisha usajili wa Jean Baleke itakuwa ngumu kuendelea kusalia, vinginevyo aonyeshe kiwango kitakachomshawishi kocha kumwamini katika kikosi chake cha kwanza,” kilisema chanzo hicho.
Kitendo cha Freddy kuonekana akifanya mazoezi na mastaa wa Yanga kama Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Yao Kouassi, kuliibua madai hayo ya kutakiwa Yanga naye alipohojiwa na chombo kimoja cha habari hapa nchini, alikakariwa akisema Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kuhitaji huduma wakati akiwa Green Eagle, kabla ya Simba kupindua meza.
Lakini alipiotafutwa na Mwanaspoti jana kuzungumzia juu ya tetesi za kutakiwa na Yanga, alikiri iliwahi kumtafuta wakati yupo na Green Eagle ya Zambia, ila kwa sasa hatapenda kulizungumzia hilo kabisa.
“Mimi ni mchezaji huru kwa sasa, nipo tayari kuitumikia klabu yoyote itakayonihitaji, ila iwe na programu nzuri ya kunifanya nizidi kucheza kwa kiwango cha juu,” alisema Freddy maarufu kama Freddy Fungafunga.